Kocha Mkuu wa Azam FC, Yossouf Dabo ameahidi kupindua meza katika mchezo wa Mkondo wa Pili wa michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya Bahir Dar Kenema ya Ethiopia.
Katika mchezo wa Mkondo wa Kwanza uliopigwa katika Uwanja wa Abebe Bikila, Ethiopia, Azam FC ilifungwa mabao 2-1 hivyo itahitaji ushindi wa bao 1-0 Uwanja wa Azam Complex mwishoni mwa juma hili kuingia Raundi ya kwanza ya michuano hiyo.
Yalikuwa ni matokeo ya kushangaza kwetu, tulikutana na mpinzani ambaye yupo imara kuliko tulivyofikiria lakini bado tuna nafasi ya kusonga mbele hatua inayofuata, tumerudi nyumbani kufanyia kazi upungufu wetu,” amesema Dabo.
Amesema wachezaji wake walipoteza umakini na kufanya makosa madogo madogo yaliyoigharimu timu hiyo na kuongeza kuwa wanarejea kwenye uwanja wa mazoezi kufanyia marekebisho mapungufu hayo.
Naye Kocha Mkuu wa Bahir Kenema, Degarege Yigzaw amesema waliingia kwenye mchezo huo wakijua uwezo waliokuwa nao wapinzani wao Azam FC na kilicho wasaidia ni kucheza kwa malengo na kutumia vizuri nafasi zao walizozipata.
Tumeshinda lakini Azam FC ni timu nzuri na tunatarajia kupata upinzani mkali kwenye mchezo wa marudiano.
“Najua watakuja kwa nguvu kutaka bao la mapema lakini mpaka siku ya mchezo, tutajua mbinu gani za kutumia ili kuwazuia na kutengeneza nafasi za mabao,” amesema Yrigzaw.
Mshindi wa jumla wa Azam FC na Bahir Kenema anatarajia kukutana na Club Africain ya Tunisia katika hatua ya Raundi ya kwanza ya michuano hiyo ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika.