Baada ya kukusanya alama sita ugenini, Kocha Mkuu wa Azam FC, Youssouph Dabo amesema wachezaji wake wameingia kwenye mfumo, na sasa ni mwendo wa ushindi.
Dabo baada ya vipigo viwili mfulululizo dhidi ya Young Africans (3-2) na Namungo FC (3-1), kikosi chake kimebadilika na kuibuka na ushindi mechi mbili mfululizo zote ugenini walianza na Mashujaa kwa ushindi wa mabao (3-0) Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma na dhidi ya Ihefu FC mabao 3-1, Uwanja wa Real Estate Mbarali.
Dabo amesema kuna mabadiliko makubwa kwenye kikosi chake na ubora ambao umeanza kuonekana unatokana na namna wachezaji wake wameanza kumuelewa nini anakitaka.
“Kikosi kimeingia kwenye mfumo sasa ni mwendo wa matokeo mazuri iwe nyumbani au ugenini lengo ni moja kufanya vizuri kujitengenezea kubwa mechi mbili mazingira ya kumaliza nafasi tatu za juu, jambo ambalo linawezekana na kama wachezaji wataendeleza ubora basi naiona timu ikiongeza ushindani kwa wapinzani:
“Tumepoteza kwa idadi kubwa mechi mbili mfululizo, nimekaa na wachezaji wangu nikawaelekeza namna ya kuipambania timu kwa kusaidiana majukumu naona imelipa kwani tumepata ushindi na kupunguza idadi ya mabao ya kufungwa.” amesema
Amesema sasa wanarudi uwanja wao wa nyumbani kuhakikisha wanapambania alama tatu nyingine dhidi ya Mtibwa Sugar, mechi itakayochezwa Novemba 23 mwaka huu.
Azam FC ipo nafasi ya pili kwenye msimamo baada ya kukusanya alama 19 ikicheza mechi tisa hadi sasa, wakishinda sita, sare moja na imepoteza miwili.