Baada ya kuwasili jijini Dar es salaam, akitokea mjini El Gouna-Misri, Kocha Mkuu wa Azam FC Abdihamid Moallin amefunguka na kutoa tahadhari kwa timu pinzani kuelekea Msimu Mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Azam FC iliweka Kambi nchini Misri ya majuma mawili kujiandaa na msimu mpya wa 2022/23, ambao utafunguliwa rasmi Jumamosi (Agosti 13) kwa mchezo wa Ngao ya Jamii kati ya Young Africans dhidi ya Simba SC, Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Kocha Moallin amesema alikuwa na majuma mawili bora nchini Misri na ameona ubora wa kila mchezaji huku akithibitisha kuwa wachezaji wageni wameweza kufiti mfumo wake haraka, hivyo kilichobaki ni ushindani.

“Kwa asilimia kubwa maingizo mapya yameongeza ubora ndani ya timu, kila mchezaji ana kitu cha tofauti, wamefanya vizuri kwenye maandalizi tuliyoyafanya,” alisema.

Azam FC itacheza mchezo wa Kimataifa wa Kirafiki dhidi ya Zesco United ya Zambia Jumapili (Agosti 14), Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es salaam.

Kenya: UN yawapongeza Wakenya kupiga kura kwa amani
Young Africans: Hatufahamu kwa nini hatukualikwa CAF