Kocha Mkuu wa Azam FC Abdihamid Moallin, amepingana na maoni ya baadhi ya wachambuzi wa Soka la Bongo wanaosema kufanya vibaya kwa timu yake kunatokana na wapinzani wao kujua aina yao ya uchezaaji ya kuanzia mashambulizi kutokea nyuma.
Baadhi ya wachambuzi Soka la Bongo wanasema wapinzani wa Azam FC wamekuja na mbinu ya kukabia juu hivyo kuutegua mtego wa kiufundi wa miamba hao wa Chamazi.
Kocha huyo kutoka nchini Marekani mwenye asili ya Somalia amesema hakubaliani na hilo, akisema wapinzani kujua aina ya uchezaji siyo tatizo hata kidogo kwa sababu hakuna namna yoyote timu itaweza kuficha hilo.
Asema kinachoitafuna timu yake kwa sasa ni kuridhika kwa wachezaji na benchi zima la ufundi baada ya mfululizo wa matokeo mazuri na kiwango bora kuanzia kombe la Mapinduzi na mechi za baada ya hapo.
“Bila shaka tunajua kwamba wapinzani mara zote watatuangalia tunavyocheza na kuja na mpango kabambe, kama ambavyo sisi pia hufanya, hiyo ni kawaida, nadhani kilicho muhimu ni kwamba ‘hatulikubali hilo.”
“Hatudhani kwamba eti hilo ni tattizo kwa sababu wametujua….kwa sababu Azam FC inachezaje? Hatuchezi aina moja tu ya mchezo. Kila mchezo tunaucheza kwa namna tofauti.”
“Ni kweli kwamba sisi ni timu inayoanzishia mashambulizi kutokea nyuma na tunacheza katikati ya mistari na vitu kama hivyo…lakini hili jambo ni kubwa zaidi ya hivyo.”
“Timu inaweza kukubia juu na mchezaji mmoja, wawili, watatu au hata wanne. Lakini wachezaji wanapokukabia juu, ndivyo mianya mingi wanaacha maeneo mengine…humo ndimo tunapswa kupitia. Mahali kwenye mianya ndipo kwenye faida.”
“Kwa hiyo siyo suala la timu kujua namna tunacheza, ni suala la sisi kuwa na imani na namna tunavyocheza na nadhani ni kuridhika kidogo kwa maana ya tunavyozichukulia mechi sisi wenyewe na tunapswa kujilaumu sisi wenyewe.” amesema Kocha Abdihamid Moallin
Azam FC ipo kwenye maandalizi ya mchezo dhidi ya Namungo FC, utakaopigwa Jumatano (Machi 16) mjini Lindi na kisha itapapatuana na Young Africans Aprili 6 Azam Complex.
Moallin anasema watajitahidi kurekebisha mapungufu hayo kwenye mchezo huo, huku akijiuzuia kuujadili mchezo dhidi ya Yanga ambao utafuata baada ya mchezo wa Namungo.
“Nadhani mechi kama hizi ni dhahiri ndizo tunacheza mpira kwa ajili yake. Tunapaswa kuecheza mechi muhimu dhidi ya Namungo ili kujitafuta upya, kwa maana ya pointi tatu za kuwania hasa ukizingatia tuna alama 25 hadi sasa.”
“Alama hizi tatu ni muhimu sana kwa timu zote mbili na nadhani zitategemea nani ana njaa zaidi. Mechi hiyi itakuwa kipimo kizuri kwetu, na baada ya hapo tunaangalia mchezo unaofuata dhidi ya Yanga.”
“Lakini kwa sasa akili hazipo kwa mchezo wa mbali…ni kwa Namungo tu kwa sababu huo ndiyo mchezo wetu unaofuata na tunaangalia tutaendaje huko na kupata alama tatu ili turudi kwenye hali yetu ya kushinda na ndipo tuangalie mchezo unaofuata.” amesema kocha huyo
Katika michezo mitatu iliyopita, Azam FC imepoteza michezo miwili dhidi ya Polisi Tanzania na Biashara United Mara huku ikitoka sare na Coastal Union, ikiw ahaijafunga hata bao moja kwenye michezo hiyo.