Kocha Mkuu wa Azam FC, Youssouf Dabo amesema bado haamini kama wachezaji wake walishindwa kucheza kwa mpango ambao walijipangia kulingana na ubora wa wapinzani wao Young Africans.

Azam FC ilipoteza mchezo wa Nusu Fainali ya kwanza ya Ngao ya Jamii juzi Jumatano (Agosti 09) katika Uwanja wa CCM Mkwakwani, huku kipigo hicho kikiwa gumzo kwa wadau wa soka nchini Tanzania kutokana na maandalizi kabambe yaliyofanywa na matajiri hao wa Chamazi.

Kocha Dabo amesema wakiwa mazoezini walijipanga vizuri kucheza kwa umakini katika mfumo wao wa 3-5-2 lakini walipokuja uwanjani vijana wake wakapoteza ubora, na kushindwa kufanya walichokikusudia.

“Bado najiuliza kipi kimewakumba wachezaji wangu, hatukucheza kama ambavyo tulijipanga kucheza tukiwa kwenye mazoezi yetu,”

“Tulifanya makosa mengi lakini pia tulikubali wapinzani wetu wacheze kwa uhuru wao na kilichoniumiza zaidi wachezaji wangu kupoteza kabisa ari ya kujiamini.

“Hatukucheza kwa ubora kabisa, ni makosa yetu lazima turudi kujitathimini hii ni mechi ya kwanza tuna ya kujipanga vizuri,” amesema Kocha Dabo

Azam FC bado ipo jijini Tanga ikisubiri mchezo wa mshindi wa tatu dhidi ya Singida Fountain Gate utakaopigwa Jumapili (Agosti 13) katika Uwanja wa CCM Mkwakwani.

Habari Kuu kwenye magazeti ya leo Agosti 12, 2023
ACT-Wazalendo, Wananchi wachangia Damu salama