Baada ya timu yake kupoteza mechi ya pili mfululizo, Kocha Msaidizi wa Azam FC, Bruno Ferry amesema wachezaji wake hawakuwa na kiwango bora lakini wataendelea kujifunza kwa sababu bado msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara unaendelea.

Azam FC ikiwa nyumbani ilikubali kichapo cha mabao 3-1 kutoka kwa Namungo FC katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es salaam Ijumaa (Oktoba 27).

Matokeo hayo yameifanya Azam FC kuendelea kubakia katika nafasi ya tatu ikiwa na alama 13 wakati Namungo FC imepanda hadi katika nafasi ya 12 ikiwa na alama sita kibindoni.

Kocha huyo amesema ili kufikia malengo wataendelea kujiimarisha na Ijumaa (Oktoba 27) walikuwa katika wakati mgumu kutokana na kupoteza pia mechi iliyopita.

“Kwanza kabisa napenda kuipongeza Namungo FC, walicheza vizuri, walionyesha kiwango bora, walipambana na walikuwa na bahati katika mechi ile, walifanikiwa katika mbinu zao,” alisema kocha huyo.

Ligi Kuu Bara inatarajia kuendelea leo Jumatatu (Oktoba 30) kwa JKT Tanzania kuikaribisha Dodoma Jiji FC wakati Prisons itawaalika Geita Gold na Kagera Sugar itawavaa Tabora United.

Safari ya Abraham mikononi mwa Mourinho
Chelsea, Liverpool zaharibu mipango SSC Napoli