Joto la pambano la Azam FC dhidi ya Young Africans litakalipigwa Jumamosi (April 06), Uwanja wa Azam Complex Chamazi linaendelea kupanda huku Kocha Mkuu Azam FC Abdihamid Moallin, akisema hana budi kubuni mbinu mpya.
Azam FC itakua mwenyeji wa mchezo huo, huku ikiwa na deni la kulipa kisasi cha kupoteza mchezo wa Duru la Kwanza kwa kufungwa 2-0, Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Kocha Moallin, amesema baada ya kikosi chake kucheza mchezo wa kirafiki dhidi ya DTB FC inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza, amebaini baadhi ya mambo ambayo yanapaswa kubadilishwa haraka ili kutimiza lengo la kupata alama tatu dhidi ya Young Africans.
Amesema alipendekeza kuchezwa kwa mchezo huo makusudi, ili kufahamu mapungufu na changamoto zilizopo kwenye kikosi chake, na amejiridhisha kuna jambo ambalo anapaswa kulifanyia kazi kabla ya kukutana na Young Africans.
“Niliwaomba viongozi mchezo mmoja wa kirafiki baada ya kukaa muda mrefu bila ya kucheza mechi baada ya ligi kusimama kupisha mechi za Kalenda ya FIFA.”
“Hivyo niliutumia mchezo huo kuangalia fitinesi za wachezaji wangu kwa ajili ya kuwaongezea wakati tukijiandaa kuwakabili Young Africans.”
“Nimeona upungufu kadhaa wa kikosi changu, hivyo nitafanyia kazi kwa siku hizi zilizobaki.” amesema Moallin.
Young Africans inaongoza msimamo wa Ligi Kuu kwa kuwa na alama 48, huku Azam FC ikishika nafasi ya tatu kwa kufikisha alama 28.