Kocha Mkuu wa Kagera Sugar Francis Baraza amempa ushauri wa bure Beki kutoka DR Congo na klabu ya Simba SC Henock Inonga Baka, baada ya kumuona akicheza kwa mara ya kwanza msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Beki Inonga alisajiliwa Simba SC mwanzoni mwa msimu huu akitokea DC Motema Pembe ya nchini kwao DR Congo, na hadi sasa amekua gumzo kubwa miongoni mwa wadau wa Soka la Bongo.
Baraza amesema Inonga ni Beki mzuri na amedhihirisha ubora wake tangu alipoanza kuonekana akiwa na Simba SC msimu huu, lakini ana mapungufu ambayo anapaswa kuyafanyia kazi ili awe bora zaidi.
Baraza amesema Inonga anapaswa kuongeza mwili kwa kufanya mazoezi maalum, ili kubeba sifa halisi ya Beki wa kati kama ilivyo kwa mabeki wengine waliozingatia kipengele cha kufanya mazoezi ya kutengeneza mwili.
“Inonga ninakiri wazi ni beki mzuri, nimebahatika kumuona akicheza akiwa na Simba SC katika michezo kadhaa, lakini ninamshauri afanye sana mazoezi ya kutengeneza mwili wake, akiwa na mwili mkubwa wa kimazoezi tofauti na sasa, ninaamini atakuwa beki bora sana,”
“Wakati mimi ninacheza soka kule Kenya nilikua Beki, nilizingatia sana mazoezi ya kutengeneza mwili na nilifanikiwa katika hilo, ndio maana hadi sasa unaniona bado ninadai! hivyo ninamshauri Inonga azingatie sana hili kwa sababu ninaona anakosa hii sifa, japo ana uwezo mkubwa kisoka. amesema Baraza.
Katika hatua nyingine Kocha Baraza amemsifia Beki mwingine wa Simba SC Joash Onyango kwa kazi nzuri anayoifanya kwenye kikosi cha Wekundu hao wa Msimbazi.
Amesema Onyango ana sifa za kipekee kwenye safu ya ulinzi ya Simba SC na amekua akicheza sana mipira ya vichwa tofauti na Inonga, ambaye ni makini sana kwenye mipira ya kunyang’anya.
“Ukiniambia upande wa mipira ya juu Onyango yupo vizuri sana kuliko Inonga, na kwa hili ninampongeza sana Onyango kwa sababu ameonyesha ni wa kipekee sana, binafsi huwa napenda sana kumtazama.” ameongeza Kocha Baraza.
Onyango na Inonga wamekuwa na ushirikiano mzuri tangu walipoanza kucheza pamoja msimu huu kwenye michunao ya ndani na nje ya Tanzania.
Onyango alisajiliwa Simba SC mwanzoni mwa msimu uliopita akitokea Gor Mahia ya Kenya, akiacha kumbukumbu ya kuwa Beki bora katika Ligi Kuu ya nchi hiyo msimu wa 2019/20.