Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Burundi ya soka la Ufukweni, Bulenge Ally amesikitishwa na wachezaji wake watatu kuondolewa muda mchache kabla ya mchezo wa kuwania kufuzu fainali za Afrika dhidi ya Tanzania uliochezwa jana Jumanne (Machi 30), kwa madai kukutwa na maambukizi virusi vya Corona.

Kocha Ally alitoa malalamiko hayo baada ya mchezo huo uliochezwa kwenye ufukwe wa Coco (Coco Beach) jijini Dar es salaam, na kushuhudia kikosi chake kikiambulia kisago cha mabao manane kwa matatu.

Kocha huyo alilalamika wachezaji wake kutolewa muda mchache kabla ya mchezo huo kuanza kwa madai vipimo vilionyesha wana maambukizi ya virusi vya Corona.

“Tanzania haikutuzidi sana uwanjani lakini ni kama morali yetu ilishuka kabla ya mchezo baada ya wachezaji wangu watatu kudaiwa wana Corona.”

“Wakati tunajiandaa na mechi muda mfupi kabla ya mchezo kuanza tukaambiwa wachezaji hao tuwaondoe kwani wanaumwa Corona hivyo ikabidi  tuwaambie wavue jezi na wacheze wengine,” amesema Ally.

Timu hizo zitakutana tena mwishoni mwa juma hili kwenye ufukwe wa Coco jijini Dar es salaam kucheza mchezo wa mkondo wa pili, ambapo Tanzania itakua mwenyeji, huku ikiwa na ushindi wa mabao manane kwa matatu waliouvuna jana.

Endapo Tanzania itaendeleza wimbi la ushindi kwenye mchezo huo, itasonga mbele kwenye fainali za mataifa ya Afrika kwa soka la ufukweni.

Kim Poulsen: Nina imani kubwa na Taifa Stars
Shamimu na mumewe wahukumiwa kifungo cha maisha jela