Kocha Mkuu wa Club Africain Bertrand Marchand, ametangaza hadharani kuwa tayari kwa mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa Mtoano Kombe la Shirikisho dhidi ya Young Africans.
Young Africans itakua mwenyeji wa mchezo huo Jumatano (Novemba 02) katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, kabla ya kwenda jijini Tunis-Tunia kwa mchezo wa Mkondo wa Pili utakaopigwa, Novemba 09.
Kocha Marchand amesema licha ya ubora wa kikosi cha Young Africans, bado haitakuwa sababu ya kikosi chake kushindwa kutinga hatua ya Makundi Kombe la Shirikisho msimu huu 2022/23.
“Young Africans ni Mabingwa katika Ligi yao msimu uliopita, nawaheshimu sana kwa hilo, licha ya kuondolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika lakini walionyesha kiwango kikubwa sana dhidi ya Al Hilal ya Sudan.”
“Kwetu sisi hautakuwa mchezo rahisi kucheza nao, tunajipanga ili kukabiliana nao katika michezo yote miwili, ninaamini mchezo utakua mgumu na mzuri tukianzia ugenini na tutamalizia hapa nyumbani Tunis.”
“Sisi hatutakuwa na sababu ya kushindwa kufanya vizuri na kushindwa kufuzu Hatua ya Makundi Kombe la Shirikisho, kiuwezo ninaamini tuna kila sababu ya kufuzu.” amesema Kocha huyo kutoka Ufaransa
Club Africain ilitinga hatua ya Mtoano Kombe la Shirikisho baada ya kuifunga Kipanga FC ya Zanzibar 7-0, huku Young Africans ikishiriki hatua hiyo kufuatia kutolewa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika kwa matokeo ya jumla 2-1 dhidi ya Al Hilal ya Sudan.