Kocha Mkuu wa Club Africain Bertrand Marchand amesema kikosi chake kipo tayari kwa mchezo wa Mkondo wa Kwanza Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya Young Africans.
Club Africain itacheza mchezo huo kuwania nafasi ya kutinga Hatua ya Makundi, ikianzia ugenini Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es salaam kesho Jumatano (Novemba 02), kisha itamalizia nyumbani kwao Tunis-Tunisia Novemba 09.
Kocha Bertrand amezungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es salaam na kusema anatarajia mchezo wao na Young Africans utakua mzuri na mgumu, kutokana na kila upande kuhitaji matokeo yatakayowavusha.
“Tulikuwa Tanzania kama mwezi mmoja uliopita kucheza na Kipanga FC, tunatarajia mchezo wetu na Young Africans utakuwa mzuri zaidi huenda kuliko ile iliyopita, kwa sababu sisi tumejiandaa na wao watakua wamejiandaa pia.”
“Tumekuja kupambana na mpinzani ambae yuko vizuri, Young Africans ni timu nzuri, ni timu bora kwa hiyo tumejiandaa kukutana na timu iliyo bora na tunahitaji kupambana kwa sababu huu mchezo ni wa nyumbani na ugenini.” amesema kocha huyo kutoka nchini Ufaransa
Katika hatua nyingine Kocha Bertrand amekiri kuwafahamu baadhi ya wachezaji wa Young Africans, huku wengine akiweka wazi aliwahi kutamani kufanya nao kazi kabla ya kusajili Tanzania.
“Namfahamu Kisinda, Mayele nilitaka kumsajili miaka miliwi iliyopita kipindi yuko AS Vita lakini akapata ofa ya kwenda Young Africans sikuwa pia katika Klabu hii [Club Africain]”
“Namjua Moloko nae alikuwa AS Vita, Young Africans ina wachezaji wazuri wa kimataifa kutoka Uganda, DR Congo Burkina Faso na Ghana.” amesema
Mshindi wa jumla katika mchezo huo atatinga hatua ya Makundi Kombe la Shirikisho Barani Afrika na kuungana na miamba mingine 15 itakayopata ushindi kwenye hatua hii ya mtoano.