Kocha mkuu wa Kikosi cha Coastal Union FC, Fikiri Elias ameweka wazi mipango yao ya kuhakikisha wanashinda michezo minne ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyosalia kabla ya kumalizika kwa msimu huu 2022/23.
Licha ya Coastal Union FC kushika nafasi ya 12 kwenye msimamo kwa alama 27 baada ya michezo 26, lakini bado inahitaji kupata ushindi katika michezo iliyosalia kwani timu nyingi zimeachana kwa tofauti ya alama chake hivyo kufanya ambaye atashuka kutojulikana hadi sasa.
Katika michezo hiyo Wagosi wameshinda michezo sita, wakitoka sare tisa na kupoteza 11 huku wakipachika mabao 22 na kuruhusu nyavu zao kufumaniwa mara 30.
Michezo ambayo imesalia kwao ni dhidi Mtibwa Sugar ambayo itapigwa Aprili 23 katika Uwanja wa Manungu Complex, mkoani Morogoro, kisha watarejea nyumbani Mkwakwani Tanga kucheza mechi mbili mfululizo dhidi ya Ihefu, Mei 14 na Azam FC, Mei 24 halafu watasafiri kumalizia ugenini Mei 28, Uwanja wa Uhuru dhidi ya Simba.
“Kwa sasa kila mechi kwetu ni fainali, ligi ni ngumu mechi zenyewe zimebaki chache na ukiangalia kwenye msimamo timu zimepishana kwa alama chache sana.” Amesema Kocha Fikiri Elias
Ametumia fursa hiyo kuwashukuru mashabiki wa timu hiyo kwa kuendelea kupambana kutoa sapoti yao kila wanapoenda kucheza kwani imekuwa ni chachu ya kufanya vijana kupambana ili kuwafurahisha.