Baada ya kupoteza mchezo wake wa pili dhidi ya Esperance de Tunis ya nchini Tunisia, Kocha Mkuu wa Azam FC, Youssoupha Dabo, ametamba kuwa ataendelea kukijenga kikosi kuikabili timu ya US Monastir.

Akizungumza baada ya mpambano dhidi ya Esperance de Tunis, Kocha Dabo alisema lengo lake ni kucheza mechi ngumu, kuhakikisha anaangalia uwezo wa kila mchezaji wake

“Nimetaka kucheza mechi ngumu kuhakikisha ninajua kikosi changu kinatakiwa kujengwa zaidi katika nafasi gani, mechi hizo zitasaidia wachezaji wangu kuwa bora na kupata uzoefu wa kutosha,” alisema.

Dabo amesema kesho Jumamosi (Julai 22) watacheza mchezo mwingine dhidi Monastir, lengo kubwa la kucheza mechi hizo ngumu ni kukijenga kikosi chake kuweza kuwa imara kwa ajili ya mashindano ya msimu ujao.

Hata hivyo, Afisa Habari wa Azam FC, Hashim lbwe amesema timu yao inaendelea na maandalizi kwa ajili ya msimu ujao na watahakikisha wanarejea wakiwa na makali zaidi.

Amesema kocha wao, ametaka mechi za kirafiki kucheza na timu ngumu ili wachezaji wake wapate uzoefu pale mashindano yatakapoanza.

“Mechi zingine ambazo tumebaki nazo ni US Monastir, Etoile Du Sahel, CS Sfaxien zote za nchini Tunisia, tunaamini tukirejea nchini tutakuwa hatushikiki,” amesema lbwe.

Azam FC iliondoka nchini Julai 9, mwaka huu, inatarajiwa kurejea nchini Julai 30, mwaka huu.

lkirejea nchini, timu hiyo itakuwa na kibarua kizito dhidi ya Young Africans katika mchezo wa Nusu Fainali ya Ngao ya Jamii utakaochezwa Agosti 9, mwaka huu katika Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Wayne Rooney ampa baraka Declan Rice
Joshua Kimmich bado yupo sana