Baada ya kupokea kisago cha 3-0, Kocha Mkuu wa Dodoma Jiji FC, Masoud Djuma Irambona ametoa sababu za kushindwa kuhimili mikiki mikiki ya Simba SC iliyokua nyumbani, Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Kocha Masoud amesema wachezaji wake walikuwa na mchoko wa safari, ambapo walilazimika kuuwahi mchezo huo wakitokea mjini Singida baada ya kucheza dhidi ya Geita Gold FC.
Hata hivyo Kocha huyo kutoka nchini Burundi amesema, wachezaji wake walicheza kwa kuiheshimu Simba SC, na kipinid cha pili walionyesha uwezo mkubwa tofauti na ilivyokua kipindi cha kwanza ambapo walikubali kufungwa 2-0.
“Kipindi cha pili wachezaji wangu walichangamka tofauti na ilivyokuwa mwanzo wa mchezo na hapo tuliwapa ushindani wa kutosha Simba SC,”
“Mchezo huo umekwisha sasa wanakwenda kufanya maandalizi na kurekebisha makosa yao kabla ya kucheza na Ihefu ili kupata matokeo mazuri tofauti na hayo dhidi ya Simba SC.” Amesema Djuma aliyewahi kuwa kocha msaidizi wa Simba SC
Wakati huo huo Ligi Kuu Tanzania Bara itaendelea tena leo kwa michezo mitatu kupigwa katika miji ya Tanga na Dar es salaam.
Mjini Tanga wenyeji Wagosi wa kaya Coastal Union wanarudi kwenye Dimba la Mkwakwani kwa mara ya kwanza Msimu huu kuwakabili Wana Super Nkurukumbi Kagera Sugar saa 10:00 Jioni.
Bingwa mtetezi wa taji la Ligi Kuu wananchi Young Africans na kipimo cha mwisho dhidi ya Ruvu Shooting kabla ya kuikabili Al Hilal ya Sudan jumamosi hii kwenye Dimba la Mkapa.
Matajiri wa Chamazi Azam FC nao watakuwa na kibarua mbele ya Wabrazil wa Singida Big Stars kwenye Dimba la Azam Complex saa 2:15 Usiku.