Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans wanaendelea kujiandaa kwa mchezo wa hatua ya kwanza ya mtoano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya El Merreikh ya nchini Sudan, lakini kocha wa Wasudan hao ametoa kauli ikionyesha jinsi gani ana pasua kichwa, huku akimtaja Pacome Zouzoa.
Kocha Osama Nabieh amesema kuwa wakati wanajiandaa kukutana na Young Africans kama kuna kitu wanapambana nacho ni jinsi gani ya kukabiliana na ufiti wa wachezaji wa wapinzani wao kutoka Tanzania.
Amesema mechi ambazo wameziona za Young Africans hivi karibuni ni lazima watafute akili ya kukabiliana na ubora wa safu ya kiungo ambayo inaundwa na Pacome, Maxi Nzengeli, Stephanie Aziz Ki wanaopishana, Khalid Aucho na Mudathir Yahya.
Nabieh amesema wanatambua timu yao inakosa kitu kikubwa kwa kutocheza mechi za ushindani kutokana na ligi yao kusimama na kuhamia nchini Rwanda ambako wanacheza mechi za kirafiki.
Juma lilopita El Merreikh ilicheza dhidi ya Rayon Sport ya Rwanda wakiambulia kipigo cha bao 1-0 ukiwa ni mchezo maalumu wa Wasudan hao wakitafuta utayari kabla ya kukutana na Young Africans.
“Wenzetu ukiangalia mechi zao wanaonekana wako tayari. Ni timu ambayo iko fiti na kitu kibaya zaidi kwetu ni kwamba wameshinda mechi za ligi na mbili za Afrika, lakini wakiwa na mastaa kama Zouzoua,” amesema Nabieh, raia wa Misri.
Tunalazimika kucheza mechi kama hizi za kirafiki ambazo sawa zinaweza kutusaidia, lakini sio kwa ukubwa kama utakapocheza mechi za ushindani kama ligi. Tutaendelea kujipanga zaidi tukiangalia kama tutapata mechi nyingine hapa karibuni ya kirafiki.
“Ubora wao mkubwa uko eneo la kiungo mechi ambazo tumeziangalia kama hatutakuwa na ubora wa kuwadhibiti eneo hilo tunaweza kufanya makosa, lakini pia kwenye ulinzi pia ni timu nzuri.
“Haitakuwa mechi rahisi kwetu na hata kwao, nimewaambia wachezaji wangu hii ni sawasawa na fainali kwetu itakayoamua safari yetu kwenye mashindano haya, tunatakiwa kucheza kama wanajeshi.”
Young Africans itakutana na El Merreikh Septemba l6 jijini Kigali mchezo utakaopigwa uwanja wa Pele (zamani ukijulikana Nyamirambo) ambapo baada ya mchezo huo timu hizo zitarudiana majuma mawili baadae nchini Uwanja wa Azam Complex – Chamnazi, Dar.