Wakati Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans wakiendelea kuboresha kikosi tayari kwa msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Kocha Miguel Angel Gamondi, ameanza kutekeleza majukumu yake kwa kuangalia sifa za wachezaji watakaobaki, kusajiliwa.
Juni 24, mwaka huu, Young Africans ilimtangaza Gamondi kuwa kocha mkuu akirithi mikoba ya Nasredine Nabi, aliyeomba kuondoka baada ya mkataba wake kumalizika.
Afisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe, amesema wakati dirisha la usajili likifunguliwa Jumamosi (Julai Mosi), klabu imempa kocha nafasi ya kutoa mapendekezo ya kuboresha timu.
Kamwe amesema pamoja na kuwa kocha bado hajawasili nchini, kazi ya kuboresha timu ameanza kuifanya akishirikiana kwa karibu na viongozi wa kamati ya usajili.
Amesema jukumu la aliloanza kufanya Gamondi ni kupitia wasifu wa wachezaji waliobaki kikosini, kuangalia video za mechi walizocheza na kutoa mapendekezo.
“Tuna mawasiliano ya karibu, viongozi wanashauriana na kocha mambo mbalimbali hasa katika kipindi hiki cha usajili, naamini tutafanya usajili makini ambao kuendelea utaiwezesha timu kutakata katika mashindano yote itakayoshiriki msimu ujao,” amesema Kamwe.
Afisa huyo amesema na usajili kuendelea, programu za pamoja maandalizi ya msimu ujao zimeanza kuandaliwa zikiwemo taratibu za kambi na michezo ya kirafiki ya ndani na kimataifa.
Hadi sasa Young Africans imewapa mkono wa kwaheri wachezaji watano ambao ni Mlinda Lango Erick Johora, Abdalah Shaibu ‘Ninja’, Benard Morison, Dickson Ambundo na Tusila Kisinda.