Kocha Mkuu wa Mpya wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans, Miguel Gamondi amepangua ratiba ya viongozi waliyoiweka kwa ajili ya Maandalizi kuelekea kwenye msimu mpya wa Ligi Kuu na michuano ya Kimataifa.
Awali uongozi huo wa Young Africans ulipanga timu ianze maandalizi Juma Lijalo kwa kwenda kuweka kambi Tunisia, lakini kocha huyo kutoka nchini Argentina amesitisha na kusogeza mbele siku ya kuanza kwa kambi hiyo.
Taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo zinasema Kocha huyo ameomba kusogezwa mbele kwa kambi hiyo na kuutaka uongozi umsubiri mpaka atakapowasili nchini.
Mmoja wa viongozi wa klabu hiyo amesema kuwa Gamondi anataka kwanza awe na wasaidizi wake ndipo waende kuweka kambi kujiandaa na msimu ujao.
“Uongozi umekubali mapendekezo yake, sasa tunasubiri aje nchini ndipo tutafahamu lini hasa timu itaanza maandalizi na wapi wataenda kuweka kambi, uongozi tulipanga kwenda Tunisia lakini tunasubiri maamuzi ya kocha, kama atapendekeza sehemu nyingine au huko huko Tunisia,” amesema Kiongozi huyo ambaye hakutaka jina lake kuanikwa hadharani.
Amesema maamuzi yote ya maandalizi ya msimu mpya wameyaacha mikononi mwa kocha wao huyo mpya aliyechukuliwa kuziba nafasi ya Nasreddine Nabi ambaye hakuongeza mkataba baada ya mkataba wake wa awali kumalizika.
“Kocha ana mapendekezo ya wasaidizi wake, sasa nadhani anataka wapatikane wasaini wote mkataba ndipo sasa maandalizi kwa ajili ya msimu mpya yaanze, uongozi tumekubali tunamsubiri,” amesema kiongozi huyo.
Alipotafutwa Msemaji wa Young Africans, Ally Kamwe amesema viongozi wamekamilisha mambo mazuri na wanamsubiri kocha wao aje ili maandalizi ya msimu mpya yaanze.
Amesema wanataka kuendeleza makali ya msimu ujao kwa kutwaa mataji yote ya ndani kama ilivyo msimu 2022/23 Young Africans ilipotwaa makombe matatu ya Ngao ya Jamii, Ligi Kuu Tanzania Bara na Kombe la Shirikisho ‘ASFC’.
“Tunamsubiri kocha wetu aje, jukumu lote la usajili liko chini yake na hata maandalizi yetu yapo chini yake,” amesema Kamwe.
Amesema katika eneo ambalo wapo makini ni la maboresho ya kikosi na wanaamini Yanga itakuwa bora zaidi ya msimu uliopita ambao walifanikiwa kutinga hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.