Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Geita, Zahara Michuzi amemtaka Kocha Mkuu wa timu ya Geita Gold inayomilikiwa na Halmashauri hiyo, Hemed Suleiman Morocco afike ofisini kwake mara moja kueleza kiini cha matokeo mabaya.

Zahara ametoa maelekezo hayo kwa kueleza kutoridhishwa na mwenendo wa timu hiyo na kulitaka benchi la ufundi lifike kumueleza kikwazo ni nini.

“Nimetoa wito na angalizo kwa Kocha wa timu ya Geita Gold FC, kwanza anione kabla sijamtafuta, yeye pamoja na benchi lake na ufundi, kabla ya hatua yoyote tunaweza tukazungumza, kujua kwamba tunakwama wapi.

“Sisi kama Halmashauri na wamiliki wa ile timu hatujawajibika wapi, labda tunamkwamisha Kocha, lakini niwahakikishieni timu ile sisi kama Halmashauri tumewajibika kadri ya uwezo wetu kuhakikisha inafanya vizuri.

“Lakini tunataka tuwasikilize na wenzetu wa upande wa pili wanasemaje, kama changamoto itakuwa ni ya kwao tutawapa angalizo la kurekebisha ile changamoto na tunataka tuone matokeo.”

Amekiri matokeo ya suluhu waliyopata Geita Gold FC ugenini mkoani Mbeya dhidi ya Tanzania Prisons yanatoa mwanga wa mabadiliko, lakini lazima hatua thabiti zichukuliwe kumaliza ukata wa matokeo mazuri.

“Kama changamoto ipo kwa wachezaji basi na kwenyewe tutachukua hatua, hakuna mkubwa zaidi ya mwajiri, na mwajiri ni Halmashauri, hakuna mkubwa yeyote kwenye timu zaidi ya mwajiri.”

Amesema na kusisitiza kuwa timu ya Geita Gold mpaka sasa ipo kwenye matazamio na yeyote atakayesumbua na kuonekana kikwazo ndani ya timu atachukuliwa hatua kulingana na makubaliano ya mikataba.

Ikumbukwe Geita Gold FC inayofundishwa na kocha Morocco ambaye tangu apewe dhamana hiyo, imecheza michezo nane ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara na kupoteza michezo minne, kupata sare tatu na kushinda mara moja.

Wazaze watakiwa kuwekeza kwenye malezi bora
Elimu ya lazima kuwa miaka 10 - Waziri Mkuu