Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa Ghana, Chris Huhton hajakata tamaa kwenye matumaini ya kumshawishi Mshambuliaji Eddie Nketiah aache kuichezea England na kuhamia Ghana kwenye soka la kimataifa.
Mshambuliaji Nketiah alizaliwa Lewisham, Kusini mwa London na alichezea timu nyingi za vijana za England na kuweka rekodi ya kuwa kinara wa mabao kwa timu ya chini ya miaka 21.
Lakini, wazazi wake ni Waghana, hivyo anakubalika kuichezea Black Stars inayonolewa na Hughton.
Hata hivyo, Nketiah mwenye umri wa miaka 24, hataruhusiwa kubadili utaifa kama ataitumikia England kwenye mechi ya kimashindano, ambapo kesho Jumanne (Oktoba 17) watakuwa na kipute cha kuikabili Italia kwenye kufuzu Euro 2024.
Hughton mwenye umri wa miaka 64, alisema: “Baadhi ya wachezaji wamekuwa wazi kila wanachotaka kukifanya. Wengine hawana uhakika na wengine wanataka kuona mambo yanavyoendelea.
“Nafikiri kitu kama hiki kipo kwenye kesi ya Eddie. Hatuwezi kukata tamaa kumshawishi ili aje Ghana. Lakini, hilo linategemea na mchezaji kile ambacho anataka.”
Hughton bado pia anapambana kuona kama Callum Hudson-Odoi naye atabadili utaifa wake, ambapo staa huyo wa Nottingham Forest mwenye umri wa miaka 22, ameshaitwa mara mara tatu kwenye kikosi cha England, lakini mara zote hizo ilikuwa 2019 kipindi hicho alipokuwa chini ya umri wa miaka 21, ambao kwa sasa si kikwazo akibadili utaifa.