Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Didier Gomes amewataka wachezaji wake kuwa tayari kwa mapambano ya kweli dhidi ya AS Vita, katika mchezo wa mzunguuko wa tano wa Ligi ya mabingwa Barani Afrika utakaochezwa April 03, Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Simba SC watakuwa wenyeji wa mchezo huo, huku wakihitaji alama moja ili kujihakikishia kufuzu hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.

Kocha Gomes amesema anaamini mchezo huo utakua na upinzani wa kweli, kutokana na hitaji la AS Vita ambayo itahitaji kushinda ili kufufua matumaini ya kusonga mbele kwenye michuano hiyo, hivyo wachezaji wake wanapaswa kupambana na kuweka mbele maslahi ya klabu na sio jambo lingine lolote.

Amesema mchezo huo utakua na sababu zote za wao kushinda, hasa ikizingatiwa wanacheza nyumbani Dar es salaam, na utakua mchezo wa mwisho hatua ya makundi kuchezwa kwenye ardhi ya Tanzania,kabla ya kuelekea Misri kumalizia mzunguuko wa mwisho dhidi ya Al Ahly.

“Nimewaambia wachezaji kwamba haitakuwa kazi nyepesi kwetu na kila timu inahitaji ushindi hivyo ni muhimu kujipanga vizuri.

“Ikiwa tutashindwa kupata matokeo itakuwa ngumu kwetu kufikia malengo ya hatua ya robo fainali hivyo tupo tayari kufanya vizuri.” Amesema Gomes.

Simba SC inaongoza msimamo wa Kundi A, kwa kuwa na alama 10, ikifuatiwa na Al Ahly yenye alama 7, huku AS Vita ikishika nafasi ya tatu kwa kumiliki alama 4 na Al Merrikh wanaburuza mkia kwa kuwa na alama moja.

Rais Mwinyi: Kiongozi kama Magufuli ni nadra kupatikana
PICHA: Picha rasmi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan