Kocha Mkuu wa Kaizer Chiefs Gavin Hunt ameanza kujiandaa kisaikolojia, kuelekea mchezo wa mkondo wa pili wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika hatua ya Robo Fainali, dhidi ya Simba SC.

Kaizer Chiefs wanatarajiwa kuwa wageni wa Simba SC, mwishoni mwa juma hili jijini Dar es salaam, Uwanja wa Benjamin Mkapa, huku wakiongoza kwa idadi kubwa ya mabao.

Hunt amesema licha ya kuwa mbele kwa mabao manne kwa sifuri, hana budi kujiandaa kikamilifu, kwa sababu anafahamu mazingira ya uwanja wa Benjamin Mpaka, ambao umekua kikwazo kwa klabu kadhaa za barani Afrika pindi zinapokutana na Simba SC.

Amesema atakiandaa kikosi chake kucheza kwa heshima zote katika uwanja huo, huku wakiamini lolote linaweza kutokea na ulimwengu ukashangazwa.

“Tunafurahi kupata ushindi huu muhimu wa mkondo wa kwanza dhidi ya Simba, lakini nikiri kuwa tuna kazi ngumu ya kulinda matokeo dhidi ya Simba tutakapokwenda Tanzania.”

“Simba ni timu bora inapokuwa nyumbani (kwa Mkapa) na tatizo kubwa kwetu ni kuwa wenzetu wana faida ya kucheza na mashabiki, jambo ambalo kwetu hatujawa nalo kwa miaka miwili sasa.” Amesema Hunt.

Msimu huu Simba SC imekua na maajabu makubwa inapocheza Uwanja wa Benjamin Mkapa, kwa kuzifunga Al Ahly ya Misri, AS Vita ya DR Congo, Al Mereikh ya Sudan pamoja na FC Platnum ya Zimbabwe, huku ikitoka sare ya bila kufungana dhidi ya Plateau United ya Nigeria.

Katika mchezo wa mkondo wa pili utakaochezwa Jumamosi (Mei 22) Simba SC italazimika kusaka ushindi wa mabao matano kwa sifuri ama zaidi, ili kujihakikishia nafasi ya kutinga hatua ya nusu fainali.

Maagizo ya Dkt Mpango kwa Wakuu wa Mikoa
Rais Samia abadilisha Wakuu wa Mikoa wawili