Kocha Msaidizi wa Ihefu FC Zubeir Katwila amemkingia kifua Mlinda Lango Fikirini Bakari Suleiman, kwa kusema hapaswi kulaumiwa kwa makosa yaliyopelekea kikosi chake kupoteza 1-0 dhidi ya Young Africans.

Mlinda Lango Fikirini alifanya makosa yaliyosababisha Mshambuliaji Fiston Mayele kuifungia Young Africans bao la ushindi dhidi ya Ihefu FC, ambayo jana Jumatatu (Januari 16), ilicheza ugenini Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Baada ya mchezo huo Kocha Katwila alisema, ni sawa na upuuzi kumrushia lawama Mlinda Lango huyo kwa kosa alilolifanya, zaidi ya kupongezwa kwa mazuri alioyafanya kwenye mchezo huo, ambayo ni mengi.

“Nafikiri amefanya mazuri mengi zaidi ya lile kosa moja, yule ni golikipa wetu na ataendelea kuwa wetu. Kosa kama lile kina sahihishwa kwenye uwanja wa mazoezi.”

“Hata wakati tukiwa mapumzikoni tulimwambia, Mayele amekuwa anakusubiri nyuma yako kabla ya kuanzisha mpira hivyo awe makini. Hata wakati anafanya lile kosa aligeuka kwanza nyuma, pengine aliona yupo mbali.”

“Hatuwezi kusema yeye ndio ahukumiwe, yule ni mchezaji na alifanya mazuri mengi ukiondoa hilo kosa.” alisema Katwila

Ushindi huo unaendelea kuiweka kileleni Young Africans kwa kufikisha alama 53 baada ya kucheza michezo 20, ikifuatiwa na Simba SC yenye alama 44, ikicheza michezo 19.

Ihefu FC iliyocheza michezo 20, imeendelea kusalia nafasi ya 13, ikiwa na alama 20.

Kocha Nabi awakataa Fei Toto, Morrison
Bernard Morrison aichokonoa Young Africans