Kocha mpya wa Ihefu, Moses Basena amesema anahitaji majuma mawili kuisuka upya timu hiyo ili kuwa na mwenendo mzuri kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.
Kocha huyo amesema hiyo ni kutokana na mapungufu aliyoyakuta kwa wachezaji na ushindani uliopo kwenye ligi ya msimu huu.
“Tuna wachezaji wazuri lakini kwa siku chache nilizokuwa hapa nimebaini ambacho ndio nakifanyia kazi kwenye mazoezi yetu, naamini baada ya muda mfupi tutakuwa tayari kuwapa furaha mashabiki zetu kila tutakapocheza,” amesema Basena.
Koha huyo ambaye amechukua nafasi ya Zuberi Katwila, amesema malengo yake ni kuifanya Ihefu kuwa timu inayopigania ubingwa na siyo kusindikiza timu nyingine.
Amesema uongozi wa timu hiyo umemuahidi kumpa kila atakachohitaji ili kutimiza lengo hilo na yeye atahakikisha anafanikisha hilo kwa kujenga kikosi imara kitakachopigania ubingwa wa ligi kuanzia msimu huu.
Amesema hilo linawezekana sababu ligi ndio imeanza hivyo ana muda wa kutosha kurekebisha mapungufu yaliyopo na kujenga kikosi cha ushindani.
Basema aliyewahi kukinoa kikosi cha Simba SC mwaka 2011, kabla ya kutua Ihefu alikuwa kocha msaidizi wa timu ya taifa ya Uganda ‘Cranes’.