Kocha Mkuu wa JKT Tanzania, Malale Hamsini amewataka wachezaji wa timu hiyo kuendelea kupambana zaidi hasa katika michezo ya ugenini na kuachana na dhana ya kujitoa tu wakati wanapokuwa nyumbani.
Kocha Malale amesema msimu huu 2023/24 umekuwa mgumu kwa kila timu hivyo jitihada zinahitajika kwa ajili ya kuendana na ushindani.
“Ligi imekuwa ngumu kwa sababu hujui ni wapi utadondosha pointi, nimekaa na wachezaji na kuwataka kupambana kwa kadri ya uwezo wao bila ya kujali kwani ugenini pamekuwa pagumu zaidi kutokana na kila timu kuhitaji kushinda nyumbani,” amesema.
Malale ameongeza kuwa baada ya ushindi wa mwisho katika mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar walioshinda kwa mabao 2-l, nguvu wanazielekeza ugenini tena wakati watakapocheza na Geita Gold kwenye Uwanja wa Nyankumbu mjini Geita, Novemba 22.
“Ni mchezo wa mtego kwa sababu siku zote unapokuwa ugenini ni lazima ujiandae kwa maana ya kiakili na kimwili na hii ni kutokana na kila timu inapigania kupata ushindi hivyo sio rahisi lakini tutaonyesha ubora tulionao. amesema
Katika michezo tisa iliyocheza timu hiyo imeshinda minne, sare miwili na kupoteza mitatu ikiwa katika nafasi ya sita na pointi 14.