Uongozi wa Simba SC una imani kubwa na Kaimu Kocha Mkuu Juma Ramadhan Mgunda ataiongoza vizuri timu hiyo na kurejesha furaha kwa mashabiki wa klabu hiyo dhidi ya Young Africans.

Kocha Mgunda atakutana na Young Africans kwa mara ya kwanza Jumapili (Oktoba 23) tangu alipotangazwa kuwa Kaimu Kocha Mkuu wa Simba SC mapema mwezi uliopita, baada ya kuondoka kwa Kocha Zoran Maki kutoka Serbia.

Meneja wa Habari na Mawasilino wa Simba SC Ahmed Ally amesema Mgunda anajua namna ya kucheza na Young Africans na amedhihirisha hili alipokuwa Coastal Union kama Kocha Mkuu.

“Tunaamini kuanzia Mashabiki, Viongozi na Wachezaji wote nguvu na akili zao wamezielekeza katika mchezo wetu wa Jumapili dhidi ya Young Africans, uziri ni kwamba tumemkabidhi jukumu hilo Kocha wetu Juma Mgunda.”

“Kocha wetu anajua namna ya kucheza na wapinzani wetu, hatuna hofu na hilo kwa sababu tunaamini kwake ataweza kukamilisha na kurejesha furaha yetu iliyopotea kwa kipindi kirefu.”

“Tunajivunia ubora wa kikosi chetu ambacho kimetufanya kuwa bora katika michezo ya Ligi Kuu kwa msimu huu hadi sasa, na pia Kimataifa kimetuheshimisha baada ya kufikia lengo la Kwanza la kutinga hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.” amesema Ahmed Ally

Msimu uliopita Kocha Juma Mgunda wakiwa na kikosi cha Coastal Union aliitoa jasho Young Africans katika mchezo wa Fainali Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’, kwa kulazimishwa sare ya 3-3 kabla ya Wananchi kushinda kwa mikwaju ya Penati, kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.

Sure Boy aondoa mashaka kambini Young Africans
Jemedari Said aipa changamoto Young Africans