Kocha Mkuu Ihefu FC Zuber Katwila amesema kuondoka ama kubaki kwakwe kwenye Benchi la Ufundi la Klabu hiyo ipo mikononi mwa Viongozi waliompa ajira miaka miwili iliyopita.
Katwila amekua na matokeo mabaya tangu kuanza kwa msimu huu 2022/23, hali ambayo imeibua minong’ono huenda akatimuliwa na nafasi yake kuchukuliwa na Kocha mwingine.
Kocha huyo ambaye aliwahi kukiongoza kikosi cha Mtibwa Sugar kama mchezaji na baadae kukabidhiwa jukumu la Benchi la Ufundi, amesema hawezi kusema chochote kwa sasa zaidi ya kusubiri hatma yake kutoka kwa viongozi wa Ihefu FC.
“Jukumu langu ni kuendelea kupambana, mambo mengine ninawaachia viongozi kwa sababu waliniajiri wao na wana uwezo wa kusema chochote kuhusu hatma yangu hapa Ihefu FC.”
“Huu ni mpira na hakuna mtu anayependa kupoteza kama inavyotokea kwetu, kila mmoja anatamani kupata matokeo mazuri. Kwa hiyo inapotokea unapoteza mchezo kila mtu anaweza kusema lolote, lakini kwa upande wangu ninawaachia viongozi.” amesema Katwila
Jana Jumatano (Septemba 07) Ihefu FC ilipoteza mchezo watatu mfululizo, ikifungungwa na Mtibwa Sugar 3-1, katika Uwanja wa Manungu Complex, mkoani Morogoro.