Kocha Mkuu wa Young Africans, Mrundi Cedric Kaze, ameahidi soka safi na lenye ushindani kwenye mchezo wa leo dhidi ya Azam FC, utakaoanza mishale ya saa moja jioni, Uwanja wa Azam Complex Chamazi.

Kocha kaze ameahidi hayo baada ya kukamilisha maandalizi ya kikosi chake, ambacho mwishoni mwa juma lililopita kilichindwa kufurukuta mbele ya Namungo FC, na kuambulia matokeo ya sare ya bao moja kwa moja.

Amesema amefanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza kwenye mchezo huo, na ana uhakika hii leo kikosi chake kitakua tofauti mbele ya Azam FC, baada ya kutambulisha mbinu mpya kwa washambuliaji wake, ili kuhakikisha wanatumia vema nafasi hususan kwenye umaliziaji.

“Kila mchezo una mpango wake, tulivyocheza dhidi ya Namungo FC, si tutakavyocheza leo dhidi ya Azam FC, najua itakuwa mchezo mgumu, Ligi ya Tanzania ina ushindani mkubwa michezo yote ni tofauti.”

“Nimefanyia kazi safu ya ushambuliaji, huku nikiendelea kuwapa majukumu viungo wangu, lakini pia kuwakumbusha mabeki kuwa makini,” amesema kocha huyo.

Azam FC inaongoza msimamo wa Ligi kuu kwa tofauti nzuri ya mabao ya kufunga na kufungwa kutokana kuwa na alama 25 sawa na Young Africans inayoshika nafasi ya pili ikifuatiwa na Simba yenye alama 23, hivyo timu yoyote itakayoibuka na ushindi leo, ndiyo itakayokaa kileleni kwa idadi kubwa ya alama, lakini sare yoyote ile ‘Wanalambalamba’ hao wa Bakhressa wataendelea kukaa kileleni kwa tofauti ya mabao.

Plateau United waahidiwa zawadi nono
Ubovu wa MV Mapinduzi II wamsikitisha Waziri