Vinara wa msiammo wa Ligi Kuu Tanzania Bara Young Africans kesho Jumamosi watarejea katika jukumu la kusaka alama tatu muhimu dhidi ya Dodoma Jiji FC, kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.

Young Africans ambao watakua wenyeji kwenye mchezo huo, walicheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Singida United Jumanne (Desemba 15) mjini Singida, ikiwa ni sehemu ya kujiandaa kuwakabili Dodoma Jiji FC inayonolewa na kocha mzawa Mbwana Makata.

Kocha mkuu wa Young Africans  Cedric Kaze, amesema mchezo wa kirafiki dhidi ya Singida United, umempa mwanga wa kuona mapungufu ya kikosi chake, hivyo ameyafanyia kazi kabla ya kutinga dimbani hiyo kesho.

“Tumejiandaa vuziri kuikabili Dodoma Jiji FC, mchezo dhidi ya Singida United tulioshinda mabao 3-0, umenisaidia sana kurekebisha mapungufu yaliokuwepo kikosini kwangu, ninaamini kesho Jumamosi tutapambana na tutafikia lengo la kuongoza alama tatu.” Amesema kocha huyo kutoka nchini Burundi.

Katika hatua nyingine kocha Kaze amesema kwa muda mfupi aliokaa nchini ameona ushindani mkubwa kwenye Ligi Kuu, na hivyo anaendelea kuwapa mbinu zaidi washambuliaji wake kuhakikisha wanashinda kila mchezo.

Amesema ana imani ligi bado ndefu, wanalazimika kuwa makini na kutorudia makosa ambayo yanajitokeza katika mechi za nyuma, ikiwamo suala la kutumia vema nafasi wanazotengeneza na umakini katika safu ya ulinzi na ushambuliaji.

“Ligi ina ushindani mkubwa, hatutadharau timu yoyote tutakayokutana nayo, hivyo tunaenda kucheza na Dodoma Jiji FC ambao sio wabaya wana kikosi kizuri na wamejipanga kutafuta alama tatu, hata sisi tunahitaji kupata alama tatu ili kufikia malengo yetu,” amesema Kaze.

Young Africans wanaongoza Msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kuwa na alama 37, wakifuatiwa na Simba SC wenye alama 32, huku Azam FC wakishia nafasi ya tatu kwa kufikisha alama 28.

Dodoma Jiji FC watakaopambana dhidi ya Young Africans kesho Jumamosi, wapo kwenye nafasi ya 9 wakiwa na alama 19.

DPP awakazia waliowekeza Qnet
Lewandowski awabwaga Ronaldo, Messi