Kocha Mkuu wa KMC FC, Abdulhamid Moallin amesema siri ya timu yake kushinda mechi tatu mfululizo ni wachezaji wake kushika mapema mbinu anazowapa katika uwanja wa mazoezi.
KMC FC iliyonusurika kushuka daraja msimu uliopita ipo nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara, msimu huu ikikusanya pointi 10 ilizozipata katika mechi tano ilizocheza hadi kufikia sasa.
Kocha huyo amesema haikuwa kazi rahisi kupata matokeo hayo katika ligi yenye ushindani kama ya msimu huu lakini wachezaji wake wamekuwa wasikivu wazuri kwa kufanyia kazi kile anachowaelekeza katika uwanja wa mazoezi.
“Siri kubwa ni uwajibikaji wa wachezaji wangu katika uwanja wa mazoezi na namna wanavyoyafanyia kazi kwa vitendo yale tunayowaelekeza lakini kingine ni usajili mzuri ambao KMC FC tumeufanya msimu huu ambao unaendana na ushindani uliopo kwenye ligi,” amesema Moallin.
Kocha huyo amesema pamoja na mwanzo mzuri lakini bado wana kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha wanaendelea kushinda mechi zijazo ili kuendelea kukaa kwenye nafasi nzuri katika msimamo wa ligi.
Amesema wakati walipofungwa na Young Africans mabao 5-0, iliwakatisha tamaa wachezaji wake lakini yeye na wenzake wa benchi la ufundi walipambana kuwajenga kisaikolojia hatimaye wamejipanga na kufanya vizuri kwenye mechi zote zilizofuata.
Moallin aliyewahi kuifundisha Azam FC, msimu uliopita ameuomba uongozi wa timu hiyo kuwa na imani naye ili aweze kutimiza ndoto za timu hiyo ambazo ni kushiriki michuano ya kimataifa msimu ujao.