Kocha Mkuu wa Liverpool, Jurgen Klopp ameshangazwa na tetesi za klabu hiyo kuwa kwenye mazungumzo na Paris Saint-Ger-main kwa ajili ya uhamisho wa mkopo wa mwaka mmoja wa Mshambuliaji Kylian Mbappe.
Mfaransa huyo amebakiza miezi 12 katika mkataba wake na miamba hiyo ya Ufaransa na amewaarifu mabingwa hao wa Ligue 1 hana nia ya kuongeza mkataba mpya.
Mbappe ameshikilia msimamo wake kwani ana nia ya kujiunga na Real Madrid lakini imeshindwa kufikia bei ambayo PSG inataka ili kumnunua staa huyo.
Kwa mujibu wa ripoti PSG ipo tayari kumruhusu kwenda kwa mkopo akacheze timu yoyote kwa msimu mmoja na itaingiza pesa.
Lakini Klopp akihojiwa na kituo cha runinga cha Sky Sports amekanusha taarifa hizo.
Klopp alicheka kidogo na kujibu: “Naweza kusema nadhani ni mchezaji mzuri sana, lakini kutokana na pesa kuwa ndefu itakuwa ngumu sana, hata hivyo, hakuna kitu kama hicho. Lakini kuna timu nyingine pengine lolote linaweza kutokea, huenda kuna timu inajiandaa na inataka kushangaza dunia ya soka, lakini kwa upande wetu sidhani kama itatokea na kama ikitokea itakuwa kwa mara ya kwanza.”