Kocha Mkuu wa Marumo Gallants ya Afrika Kusini, Dylan Kerr amesema anakuja Tanzania kupambana na Young Africans huku akifahamu ubora wa mashabiki walionao ikiwa ni miongoni mwa silaha za timu za Tanzania.

Marumo wanatarajia kuvaana na Young Africans kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika itakayopigwa Mei 10, mwaka huu Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Kerr aliyewahi kuinoa Simba SC msimu wa 2015-16 amesema si mechi rahisi kwao kulingana na ratiba ngumu waliyonayo hivi karibuni hasa kwenye Ligi Kuu Afrika Kusini ambapo wanapambana kusalia kwenye ligi hiyo.

“Binafsi niseme nimeguswa na kuja kwangu tena Tanzania kutokana na ushirika wangu na Simba SC nilipokuja kuifundisha wakati huo na ni muda mzuri pia kurejea Tanzania kwa sasa.”

“Tutakuja kupambana, kufanya kile tulichokifanya kwenye mechi tisa tulizocheza ndani ya siku 28, ni ratiba ngumu tuliyoipitia hasa kwenye ligi lakini nilipofika hapa (Marumo) mara ya kwanza tulionesha kupambana na mpaka hapa tulipofika wachezaji wamefanya kazi kubwa, naamini tutaendelea kupambana,” amesema Kerr.

Kocha huyo raia wa Uingeeza amesema anafahamu upinzani wa mashabiki uwanjani atakaokutana nao kutokana na ubora wa ushangiliaji wa mashabiki wa timu za Tanzania akifafanua wamekuwa na utofauti na wa timu nyingine Afrika.

Niseme mashabiki wa Afrika wamekuwa tofauti kila kanda, Kaskazini wana aina yao kali ya ushangiliaji, sitaki kuwakosea heshima wengine lakini mashabiki wa Simba SC na Young Africans wamekuwa na ushangiliaji mzuri na wa kuvutia mno dhidi ya wapinzani,” amesema Ker

Pia aliongeza kuwa timu za Tanzania zinaelekea kwenye mafanikio makubwa Afrika kutokana na uwekezaji uliopo kwenye sekta hiyo akilinganisha na wakati ambao anaiona Simba SC, akikiri kwa sasa hali ni tofauti.

Marumo inatarajia kurudiana na Young Africans Mei 17, mwaka huu kwenye Uwanja wa Royal Bafokeng Rustenburg, mchezo unaotarajia kupigwa kuanzia saa 1.00 usiku.

Robertinho ampitisha Nyoni, ataja sifa nne
Guardiola: Philips ameshikilia hatma yake