Kocha Mkuu wa Marumo Gallants Dylan Kerr amesema ana uhakika mkubwa wa kupata matokeo katika Mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa Nusu Fainali ya Kombe Shirikisho Barani Afrika dhidi ya Young Africans kwa kuwa atapata sapoti kubwa kutoka kwa Simba SC.
Marumo Gallants itaanzia ugenini jijini Dar es salaam katika uwanja wa Benjamin Mkapa kuikabili Young Africans Mei 10, kabla ya kumalizia mchezo wa Mkondo wa Pili ambao utapigwa Afrika Kusini katika Uwanja wa Dobsonville, Mei 17.
Kocha huyo kutoka England ambaye aliwahi kukinoa kikosi cha Simba SC amesema kuwa anakuja Tanzania kwa kazi ya kuhakikisha wanapata matokeo ya ushindi huku akaimini atapata sapoti kubwa kutoka kwenye klabu yake ya zamani ambao ni wapinzani wakubwa wa Young Africans.
“Binafsi hatuna presha ya mchezo wetu na Young Africans kwa sababu nawajua vizuri na tayari tumeanza kuwafuatilia kupitia watu wetu lakini siyo mgeni na Tanzania kwa kuwa tayari nimewahi kufanya kazi na Simba SC ambao ni familia yangu, malengo yetu kama timu ni kuona tunashinda kwa kupita kila hatua ya michuano hii mikubwa Afrika.”
“Naamini matokeo ya ushindi ambayo tunatarajia kuyapata katika mchezo wa kwanza Tanzania, yatachagizwa na Simba SC pamoja mashabiki wao kwa sababu itakuwa ni furaha kubwa kuona tumewafunga wapinzani wao licha ya kwamba tunapita katika kipindi kigumu katika ligi ya nyumbani kwa kupambania kubakia katika ligi kuu lakini hatuwezi kusitisha malengo,” amesema Kerr
Marumo Gallants ilitinga Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika kwa kuifunga Pyramid ya Misri kwa ushindi wa jumla wa 2-1, huku Young Africans ikiitupa nje Rivers United ya Nigeria kwa ushindi wa jumla wa 2-0.