Baada ya kucheza mechi tazo za Ligi Kuu Tanzania Bara, Kocha Mkuu wa Mashujaa FC Mohammed Abdallah ‘Bares’ amesema anaridhishwa na mwenendo wa timu yake ambayo inashiriki kwa mara ya kwanza katika ligi hiyo.
Mashujaa FC iko katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa imejikusanyia pointi nane baada ya kushinda mechi mbili na sare mbili.
Kocha Mohammed Abdallah ‘Bares’ amesema anaamini timu yake itaendelea kupambana ili kusaka matokeo bora na hatimaye kufikia malengo.
Hata hivyo Bares amesema timu yake bado haina uwezo wa kumaliza katika nafasi mbili za juu katika ligi hiyo ambazo zinatolewa ‘macho’ na vigogo wa soka nchini, Simba SC na Young Africans.
Kocha huyo amesema kikosi chake kina uwezo wa kumaliza msimu katika nafasi ya tatu au ya nne endapo wachezaji wake wataendelea kujituma na kupambana.
“Ligi ni ngumu lakini hatupaswi kuacha kuweka mikakati yetu, awamu ya kwanza ya mechi tano tumefanikiwa na sasa mechi tano za awamu ya pili tukusanye alama zote 15 au nane kama tulivyofanya awamu ya kwanza.
Katika kuhakikisha tunafanikiwa malengo yetu, tunalazimika kutafuta matokeo chanya kila mechi, ikiwa tunacheza ugenini au nyumbani, kwa sasa tunajiandaa dhidi ya Coastal Union, baada ya hapo tunaangalia ratiba kama tutacheza na Simba SC au nani,” amesema kocha huyo
Ameongeza licha ya Coastal Union kuanza vibaya msimu, wao hawatabweteka na watajiimarisha ili kuwavaa mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara mwaka 1988.