Mashabiki wa soka mkoani Mbeya wameshushwa Pesha kuelekea mchezo wa Mkondo wa Pili wa ‘Play Off’ Ligi ya Championship kati ya Mbeya City dhidi ya Mashujaa FC, ambao utaamua nani anapanda Daraja na kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao 2023/24.
Mchezo huo ambao awali ulipangwa kuchezwa jana Alhamis (Juni 22) kwenye uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, sasa utachezwa kesho Jumamosi (Juni 24) kwenye Uwanja huo, huku Mashabiki wa mkoani Mbeya wakiwa na mashaka ya kuipoteza timu yao kufuatia matokeo ya mchezo wa Mkondo wa Kwanza, ulioshuhudia Mashujaa FC ikiibuka na ushindi wa 3-1 katika Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma Jumatatu (Juni 19).
Kocha Mkuu wa Mbeya City, Abdallah Mubiru amesema kutokana na maandalizi waliyoyafanya kuelekea kwenye mchezo huo, anaamini kikosi chake kitapambana na kupata matokeo mazuri yatakayowarudisha Ligi Kuu msimu ujao 2023/24.
Mubiru amesema wamefanyia kazi mapungufu waliyoyaona kwenye mchezo uliopita na wamewasoma vizuri wapinzani wao ambao walikuwa walicheza kwa kujiamini katika Uwanja wao wa Lake Tanganyika.
“Nina imani kubwa kuelekea mchezo wetu wa marudiano, tumeona ubora wa wapinzani wetu, makosa ambayo tuliyoyafanya kwenye mchezo wa kwanza tumeyafanyia kazi, tumejiandaa vizuri na tutatumia faida ya kucheza nyumbani kupata ushindi mzuri utakaotubakisha Ligi Kuu,” amesema Mubiru.
Amesema moja ya sababu ya kupoteza mchezo wao wa kwanza ni uchovu kwa wachezaji wake kutokana na kucheza mechi za mfululizo.
“Uchovu ulichangia, lakini kwenye mchezo wa kesho Jumamosi (Juni 24) hatutakuwa na Abdulrazaki Hamza ana matatizo ya kifamilia na Richardson Ng’ondya bado tutaendelea kumkosa ana matatizo ya kiafya, pamoja na yote bado ninao wachezaji wa kunipa ushindi kwenye mchezo huu,” amesema Mubiru.
“Naweza kusema wote tunajiamini, wachezaji wameahidi kufanya kazi nzuri huku wakijua kwamba ni ‘last chance’ ya kubaki kwenye ligi hivyo ni suala la kusubiri mechi ifike” amesema.
Katika mchezo huo wa kesho Jumamosi (Juni 24), Mbeya City inahitaji ushindi wa kuanzia mbaoa 2-0 kuweza kurejea Ligi Kuu, kinyume na matokeo hayo itashuka Daraja na kuwapa nafasi Mashujaa FC kupanda Ligi kuu kwa mara ya kwanza.