Kocha Mkuu wa Mbeya City, Mubiru Abdallah amesema wamekuwa na muda mzuri wa kujiandaa na kusahihisha makosa, hivyo mchezo dhidi ya Geita wanatarajia ushindi ili kufufua matumaini ya kubaki salama Ligi Kuu.
City haipo katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa michuano hiyo ikiwa nafasi ya 13 na pointi 27, kesho Jumamosi itakuwa ugenini kunyooshana na Geita Gold, mchezo utakaopigwa Uwanja wa Nyankumbu mjini Geita.
Baada ya mechi hiyo timu hiyo itarudi nyumbani Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya kucheza dhidi ya Young Africans na kuhitimisha na KMC, mechi utakaopigwa katika Uwanja wa Nelson Mandela mkoani Rukwa.
Mubiru amesema wamekuwa na muda mzuri wa maandalizi, hivyo wanaenda kwa hesabu kali kuhakikisha mechi hiyo wanashinda ili kurejesha ari na morali kikosini lakini ikiwa ni tokaeza mechi.
Amesema wachezaji wamekuwa na mwendelezo mzuri kwenye mazoezi, hali ambayo inaongeza kujiamini akiwaomba mashabiki kutokuwa na presha kubwa bali kuisapoti ili kufikia malengo.
“Tunaenda kwa umakini na tahadhari kwani wapinzani wametoka kupoteza mechi kama ilivyo kwetu, tuliona upungufu na tumeweza kuufanyia kazi na matarajio yetu ni kushinda mchezo huo na kujiweka pazuri,” amesema Mubiru.
Kocha huyo raia wa Uganda amesema baadhi ya maeneo aliyoona kukosa umakini ni ushambuliaji walioshindwa kutumia nafasi kwenye mechi zilizopita lakini beki yake nayo iliruhusu mabao.
“Tunazo mechi tatu ambazo zinatuumiza kichwa, lakini niwahakikishie mashabiki Mbeya City haishuki daraja na tunajipanga kuvuna alama tisa na tutaki salama,” amesema kocha huyo