Kaimu Kocha Mkuu wa Simba SC amesema hana budi kukubaliana na matokeo ya 1-1 dhidi ya Kegera Sugar, na sasa anaangalia mchezo unaofuata dhidi ya KMC FC utakaopigwa Jumatatu (Desemba 26) jijini Mwanza.
Simba SC ilitanguliwa kufungwa bao la mapema na wenyeji wao kupitia kwa Deus Bukenya dakika ya 15, kabla ya Simba SC kusawazisha kwa bao la kichwa lililofungwa na Beki kutoka DR Congo Enock Inonga Baka dakika ya 39 Kipindi cha Kwanza.
Kocha Mgunda amesema walicheza na mpinzani mzuri na kilichopatikana ni halali kwa kila upande, hivyo ni jambo la kipuuzi kwa mtu yoyote anayependa Soka kushindwa kuamini kilichotokea kwenye mchezo huo.
Hata hivyo Kocha huyo amesema ameona mapungufu katika mchezo huo na ameahidi kuyafanyia kazi kabla ya mchezo ujao dhidi ya KMC FC, na amesisitiza kikosi chake kuendelea kupambana hadi mwisho wa msimu huu.
“Mchezo wa Soka ni mchezo wa makosa, tumefanya makosa wenzetu wakatuadhibu dakika za mwanzoni, hata sisi tulitumia makosa yao tukasawazisha, baada ya hapo mchezo ulionekana kuwa sawa, japo tulijitahidi kutafuta matokeo mazuri lakini bahati haikuwa kwetu.”
“Mapungufu yapo na nimeyaona, kwa hiyo ninaahidi kwa kushirikana na wenzangu wa Benchi la Ufundi tutayafanyia kazi kabla ya mchezo wetu unaofuata ambao tutacheza Jumatatu (Desemba 26), jijini Mwanza dhidi ya KMC FC.”
“Bado tupo katika harakati za kutimiza wajibu wetu msimu huu, msimu haujaisha na yanayotokea ni sehemu ya mchezo wa soka, haya yanaweza kutokea hata kwa wenzetu, kwa hiyo tunachopaswa kuzingatia hivi sasa ni kuendeleza mapambano ili kufikia malengo yetu.” amesema Kocha Mgunda
Wakati huo huo Kikosi cha Simba SC kimeanza safari ya kurejea jijini Mwanza tayari kwa maandalizi ya mchezo wa Mzunguuko wa 18 wa Ligi Kuu dhidi ya KMC FC.
Simba SC imeondoka mjini Bukoba mkoani Kagera mapema leo Alhamis (Desemba 22), kwa usafiri wa basi.