Kocha Fred Felix ‘Minziro’ amegeuka lulu sokoni akitakiwa na timu zaidi ya tatu za Ligi Kuu, baada ya kumalizana na Uongozi wa Geita Gold FC kwa kukamilisha mkataba wake na kushindwa kufika makubaliano.
Timu hizo zilizoingia vitani kutaka saini ya Minziro, ni Namungo FC yenye mpango wa kuachana na Denis Kitambi, Mbeya City inayopanga kumwagana na Abdallah Mubiru na timu iliyopanda daraja msimu huu ya Tabora zamani ikiitwa Kitayosce iliyo mbioni kuachana na Henry Mkanwa.
Hadi sasa Tabora United kabla ya kubadilishwa jina ndiyo inaongoza mbio za kumpata Minziro kutokana na kutumia ushawishi wa baadhi ya viongozi wa timu hiyo ambao ni marafiki wa kocha huyo.
Mbeya City ni kama imetega tu kwani kabla ya msimu kumalizika ilikuwa na asilimia kubwa ya kumnasa Minziro na mazungumzo yalikuwa yameanza lakini baada ya kushindwa kusalia kwenye ligi na kulazimika kucheza mechi za Mtoane ‘Play Offs’ na Mashujaa ya Kigoma ambapo mchezo wa kwanza ilipoteza kwa kufungwa 3-1, na kulifanya dili hilo likisubiri miujiza ya timu hiyo.
Mbeya City inaamini kwa namna ilivyofanya mazungumzo na Minziro yalipokuwa yamefika, basi kama watabaki Ligi Kuu wanaweza kumpata kocha huyo anayesifika kwa mbinu na mazoezi magumu.
Aidha Namungo FC ipo kwenye mpango wa kupunguza gharama na kutaka kutumia zaidi wachezaji wazawa, na katika mpango huo imemuona Minziro ndiye anafaa kuutekeleza kwani amekuwa akiwatumia wachezaji wa bei rahisi kufanya vizuri katika baadhi ya timu alizopita ikiwemo Geita.
Hata hivyo, licha ya kumfuata Minziro lakini hadi tunaingia mitamboni hakuna mkataba ulikuwa umesainiwa baina ya pande hizo mbili.
Alipotafutwa Minziro kuzungumzia ni wapi anaenda baada ya Geita amesema kwa sasa anahitaji utulivu na mambo yakikaa sawa tutajulishwa.
“Naomba kupumzika kidogo, maisha lazima yaendelee na kila kitu kikikaa vizuri mtajua wapi naenda,” amesema kocha huyo aliyewahi kucheza Young Africans kama beki wa kulia akisifika kwa kukaba na kushambulia na kupiga mipira iliyokufa maarufu kama ‘Banana Chop’.
Minziro ni mmoja kati ya makocha wazawa waliopandisha timu nyingi Ligi Kuu.