Klabu ya Simba SC inatajwa kumalizana na aliyekua Kocha Msaidizi wa Mabingwa wa Soka Barani Afrika Wydad Casablanca Mohamed Benchirifa, hivyo muda wowote atatambulishwa.
Simba SC ipo kwenye mchakato wa kumsaka Kocha Mkuu ambaye atakuja kufanya kazi na Wasaidizi Juma Mgunda na Seleman Matola, ambao walifanikiwa kuivusha Klabu hiyo hadi Hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa Barani Afrika msimu huu 2022/23.
Kocha huyo alikuwa msaidizi wa Walid Regragui katika kikosi cha Wydad Casablanca ya Morocco kuanzia Januari mwaka 2021, na amekuwa hana timu tangu Novemba 02 mwaka huu 2022.
Regragui ndiye Kocha ambaye kwa sasa yupo na kikosi cha Morocco kilichofuzu Robo Fainali ya Kombe la Dunia 2022, Michuano inayoendelea nchini Qatar.
Alipotafutwa Meneja wa Habari na Mawasilino wa Simba SC Ahmed Ally kuhusu ujio wa Kocha huyo, alisema mchakato wa kumsaka Kocha Mkuu unaendelea na amewataka Wanasimba kuendelea kuwa na Subra, licha ya Tetesi nyingi kuelekezwa klabuni kwao kwa sasa.
Amesema Simba SC inafanya kazi zake kiweledi na haiwezi kukurupuka hasa katika suala la Kocha Mkuu, hivyo wakati utakapowadia taarifa rasmi zitatangazwa kupitia vyanzo mbalimbali vya habari vya Klabu hiyo Kongwe katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
“Mchakato wa Kocha Mkuu bado unaendelea na ukishakamilika muda wowote kuanzia sasa tutawatangazia Wanachama na Mashabiki wetu wa Simba SC.”
“Tumekua tunafanya kazi zetu kiweledi, hatukurupuki, ninaamini Uongozi unapaswa kufanya mazuri kwa ajili ya Wanasimba wote, kwa hiyo niwasisitize Wanasimba wenzangu waendelee kuwa na Subra, Kocha Mkuu atakuja na atatangazwa rasmi katika vyanzo vyetu mbalimbali vya habari vya Klabu yetu.”
Kocha Mohamed Benchirifa anayetajwa kumalizana na Simba SC alizaliwa Juni 23, 1976, kwa sasa ana umri wa miaka 46, wakati yupo Wydad Casablanca alimfundisha Mtanzania Simon Msuva, ambapo msimu wa 2020/21 walibeba ubingwa wa Ligi Kuu ya Morocco.