Kocha Mkuu wa Namungo FC, Hemed Morocco, amesema nguvu na mikakati kwa sasa amevihamishia kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya Al Rabita FC ya Sudan Kusini.

Mchezo wa mkondo wa kwanza kwa timu hizo utachezwa Jumamosi (Novemba 28), katika Uwanja wa Azam Complex Chamazi-Dar es salaam, kabla ya timu hizo kurudiana nchini Sudan Kusini kati ya Desemba 4-6, mwaka huu.

Kocha Morocco ambaye amechukua nafasi ya kocha kutoka nchini Burundi Thierry Hitimana aliyetimuliwa mwishoni mwa juma lililopita kutokana na matokeo mabaya ya timu hiyo, amesema licha ya kutopata nafasi ya kuwaona wapinzani wao, ana imani na uzoefu alionao katika michuano ya kimataifa atapambana ili kufanya vizuri kulingana na kikosi alichokuwa nacho.

Amesema kikubwa ambacho anakifanya ni kuangalia wachezaji ambao alionao kwa sasa pamoja na aina ya mazoezi atakayowapa kuelekea mechezo huo, ambao utakua wa kwanza kwa Namungo FC katika ngazi ya kimataifa.

“Sina presha juu ya michuano hiyo, licha ya kutopata nafasi ya kuwaona wapinzani wetu, nina uzoefu mkubwa wa michuano ya CAF, kilichobaki kwa sasa ni kuwajenga kisaikolojia wachezaji wangu ili kuachana na matokeo ya Yanga na kuelekeza akili kwenye michuano hiyo,” amesema Morocco.

Amesema tatizo la Namungo FC aliloliona kabla ya kukutana na Young Africans, wakati akifuatilia Ligi Kuu Tanzania Bara lilikuwa ni umaliziaji kwenye safu ya ushambuliaji, hivyo atalifanyia kazi.

“Kuna makosa madogo madogo kwa mabeki ikiwamo kutokuwa makini katika mipira ya faulo pamoja na kona, hilo lilitugharimu kwenye mchezo wetu dhidi ya Young Afrcans kwa kuruhusu bao kabla ya kujipanga na hatujasawazisha,” amesema Morocco.

Hii ni mara ya kwanza kwa Namungo FC kushiriki michuano ya kimataifa, baada ya kumaliza kama mshindi wa pili kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho (ASFC) kufuatia kufungwa na Simba SC mabao mawili kwa moja mjini Sumbawanga mkoani Rukwa.

Ajali yaua wanane Bukoba
Habari kubwa kwenye magazeti leo, Novemba 24, 2020