Kocha mpya wa Singida Big Stars, Emst Middendorp ameanza kazi huku akisisitiza anataka kuwaona wachezaji wake wakiwa na ukakamavu kwani kiu yao ni kuiwezesha timu hiyo kufanya vizuri mbele ya Future ya Misri na kutinga makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, licha ya ugeni katika michuano hiyo.
Singida imetinga raundi ya pili ya michuano hiyo baada ya kuing’oa JKU ya Zanzibar kwa jumla ya mabao 4-3 na itavaana na Future mwishoni mwa juma lijalo jijini Dar es Salaam kabla ya kurudiana nao ugenini na mshindi wa jumla atatinga makundi kutokana na kufutwa kwa mechi za play-off zilizokuwapo timu zikivuka raundi ya sasa.
Kocha huyo Mjerumani amenekana wazi kuwafungia vioo wachezaji ambao walikuwa wakitaka huruma yake kama msimamizi wa mazoezi pindi ambapo wanafanyiwa madhambi na badala yake aliwataka wanyanyuke ili kuendelea na mazoczi ambayo yalikuwa yakifanyiwa kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam.
Middendorp kwenye mazoezi hayo aligawa vikosi viwili na kuvishindanisha ikiwa ni mpango wa kuona uwajibikaji wa mchezaji mmoja mmoja kwenye kikosi chake ambacho kina kibarua kizito Septemba 17 kwenye Raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Wakati wachezaji wengine wa kikosi hicho wakijifua vilivyo mshambuliaji Thomas Ulimwengu na beki wa kati Abdulmajid Mangalo walikuwa na programu maalumu.
Wachezaji hao wawili walifanya mazoezi nje ya uwanja kwa sababu mbili tofauti. Taarifa za ndani zinasema, Thomas hakuwa pamoja na wenzake kambini ndio maana hakujumuishwa na wenzake kwenye mazoezi ya mpira na Mangalo ametoka kuwa majeruhi.