Shirikisho la Soka Tanzania ‘TFF’ limethibitisha kuwa kwenye mchakato wa kumsaka Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ ambayo bado ipo kwenye mbio za kusaka nafasi ya kushiriki Fainali za Afrika ‘AFCON 2023’ zitakazounguruma nchini Ivory Coast.
TFF ipo kwenye mchakato huo baada ya kumweka pembeni Kocha Kim Poulsen na nafasi yake kuchukuliwa kwa muda na Kocha Hanour Janza aliyekua anakinoa kikosi cha Namungo FC, kabla ya kurejea nchini kwao Zambia na kuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa ZESCO United.
Mkurugenzi wa Ufundi wa ‘TFF’ Oscar Mirambo amesema wapo kwenye mchakato wa kumsaka Kocha Mkuu mpya, na huenda wakamtangaza kabla ya mwezi Machi mwaka 2023.
Amesema kwa sasa kinachoendelea ni kuchuja majina ya makocha walioomba nafasi, ili kumpata Kocha ambaye atakidhi vigezo vilivyowekwa na Shirikisho hilo.
“Tunaendelea kuchakata majina ya makocha na kujua mwalimu wetu atakuwa nani. Muda wa kutangaza jina ukifika tutatangza. Makocha wameanza kutuma CV zao.”
Tunachojaribu kutazama ni mahitaji yetu binafsi ili tujue tunaenda kuwa na mwalimu wa namna gani. Tutamtangaza mwalimu kabla ya March 2023 ” amesema Oscar Mirambo kupita kipindi cha Sports HQ cha EFM Radio
Katika harakati za kuwania Tiketi ya kushiriki ‘AFCON 2023’ Taifa Stars imepangwa Kundi F na tayari imeshapoteza dhidi ya Algeria kwa kufungwa 2-0, ikitangulia kutoa sare ya 1-1 dhidi ya Niger.
Taifa Stars itaendelea na Mchakato wa kusaka nafasi ya AFCON 2023, kwa kukutana na Uganda ugenini Machi 20.
Timu hizo zitakutana tena Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam Machi 28, Kisha itaendelea kuwa nyumbani kwa kuikabili Niger Juni 12 na Mwezi Septemba itakwenda Algeria kumaliza mchakato wa kuwania kufuzu AFCON 2023.