Baada ya kupoteza mchezo uliopita, Mtibwa Sugar imesema leo Ijumaa (Novemba 03) inaenda kupambana kufa na kupona kuhakikisha wanapata pointi tatu dhidi ya JKT Tanzania na kujinasua mkiani, huku mastaa wakionywa kitu.

Mtibwa Sugar ilipoteza mechi iliyopita kwa bao l-0 dhidi ya KMC walipocheza ugenini, ambapo leo ljumaa itakuwa uwanja wa Manungu kuwakaribisha Maafande hao katika muendelezo wa Ligi Kuu raundi ya tisa.

Hata hivyo timu hizo zinakutana ikiwa kila upande unakumbuka kipigo, ambapo JKT Tanzania nao wakiwa nyumbani uwanja wa Azam walilazwa bao 1-0 dhidi ya Dodomna Jiji.

Hadi sasa JKT Tanzania wapo nafasi ya sita kwa pointi 11, huku Mtibwa Sugar wakiwa mkiani kwa alama tano na kufanya mchezo huo kuwa wa vita nzito ya pointi tatu haswa kwa wenyeji.

Kocha mkuu wa timu hiyo, Zuberi Katwila amesema licha ya kupoteza mechi iliyopita lakini vijana wake walionesha soka safi isipokuwa haikuwa bahati kwao kupata ushindi akiwatahadharisha umakini.

Amesema mchezo huo hautakuwa rahisi kutokana na wapinzani walivyo akiwataka mastaa wake kupambana kufa na kupona kuhakikisha wanabaki na ushindi ambao utawatoa mkiani.

“Ni mchezo mgumu lakini wenye umuhimu wake lazima wachezaji wapambane kadri ya uwezo wao na sisi benchi la ufundi tumerekebisha makosa hivyo matarajio ni ushindi.” amesema kocha huyo ambaye ni mechi yake ya tatu.

Erik ten Hag atahadharishwa Man Utd
Emiliano Martinez: Mbappe ni shujaa ajaye