Kocha Mkuu wa Mtibwa Sugar, Zuberi Katwila ameanza kuzipigia hesabu pointi 12 katika michezo minne ya ugenini inayofuata ya Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo ni sawa na dakika 360.
Mtibwa Sugar watakuwa ugenini wakianza dhidi ya Azam FC mchezo utakaopigwa Novemba 24 na baada ya hapo itafunga safari kuwafuata Tabora United Desemba mosi.
Wakimalizana na Tabora United watasafiri kwenda Mkoani Lindi kucheza na Namungo FC kwenye uwanja wa Majaliwa, Ruangwa Desemba 7 na siku tatu baadae watakuwa na kibarua cha kuwakabili Youing Africans kwenye uwanja wa Azam Complex, Chamazi.
Katwila amesema malengo yao ni kutafuta alama tatu kila mechi ili kujiondoka katika nafasi ya mwisho kwenye msimamo wa ligi hiyo ambayo wapo sasa.
Amesema anafahamu michezo hiyo haitakuwa rahisi lakini wamejipanga kuhakikisha wanavuna alama ili kujiondoa katika nafasi mbaya waliyopo sasa kwenye msimamo wa Ligi Kuu.
“Ligi ni ngumu na ukizingatia tumecheza michezo tisa na hatujafanya vizuri, tumeona madhaifu yetu na kwa sasa tuko uwanja wa mazoezi kujiandaa vizuri na kufanyia kazi mapungufu yetu ili tukienda kwenye mechi tusirudie makosa ambayo yalitugarimu awali.
“Mikakati yetu kwa sasa ni kushinda na kutafuta pointi katika hizo mechi ili kuweza kukusanya alama tatu au moja, kwa sababu hakuna mechi rahisi unapojiandaa na mpinzani wako naye anajiandaa,” amesema Katwila.
Mtibwa Sugar ipo mkiani katika msimano wa ligi ikiwa imekusanya alana tano tu katika michezo tisa ambayo imechezwa mpaka sasa wakishinda mchezo mmoja, sare mbili na kufungwa michezo sita.