Kocha Mkuu wa Mwadui FC Khalid Adam amesema kikosi chake kitapambana kufa na kupona kwenye mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Young Africans kesho Jumamosi (Desemba 12), ili kufanikisha ushindi wakiwa nyumbani mjini Shinyanga, kwenye Uwanja wa CCM Kambarage.

Mwadui FC wamekua hawana matokeo mazuri msimu huu, kufuatia kupoteza michezo10, tangu walipoanza kampeni za kusaka ubingwa wa Tanzania Bara mwezi Septemba 2020, lakini kocha Khalid Adam, amesema wachezaji wake wana nafasi ya kurekebisha makosa na wakarejea kwenye njia sahihi ya ushindi.

Amesema wamejiandaa kikamilifu kuelekea mchezo wa kesho, anaamini utakua mgumu kwao na kwa wapinzani wao (Young Africans), lakini akasisitiza wao watakua na faida kubwa ya kusaka matokeo kutokana na kuwa nyumbani hiyo kesho.

Kocha huyo mzawa  ameongeza kuwa, Young Africans ambao tayari wameshawasili mjini Shinyanga wataingia uwanjani huku wakifahamu udhaifu wa Mwadui FC kulingana na yaliyowafika kwenye michezo iliyopita, lakini kwake hadhani kama hilo linaweza kuwanyong’onyesha na kujikuta wakipoteza mchezo huo.  

“Watakuja wakiamini Mwadui tumeshapoteza mwelekeo, ila tunawakumbusha wajipange, tunajua tuko katika nafasi mbaya kwenye msimamo, tunahitaji kuondoka hapa tulipo, ushindi katika mechi ya Jumamosi unawezekana, ndio malengo yetu,” amesema kocha Khalid.

Ameongeza kuwa, wachezaji wake wote wako fiti na wameahidi kufanya kile wanachokihitaji katika mchezo huo, ambao utaanza mishale ya saa kumi jioni.

“Tunashida na alama tatu, kwetu ni muhimu sana, tumejipanga kupambana na tuko tayari kwa ajili ya kusaka ushindi, tunasema tutapambana.” amesema kocha Khalid.

Mwadui FC wapo nafasi ya 17 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara wakiwa na alama 10 zilizotokana na kucheza michezo kumi na nne, wameshinda michezo mitatu na kutoka sare mara moja.

Young Africans wanaongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara wakiwa na alama 34 zilizotokana na kucheza michezo kumi na nne, wameshinda michezo kumi na kutoka sare mara nne.

Young Africans wavamia Shinyanga, Kaze aahidi ushindi
Mwigizaji Tommy afariki

Comments

comments