Saa 48 baada ya Uongozi wa Young Africans kuthibitisha kuachana na Kocha kutoka nchini Tunisia Nabi Nasreddine, Kocha huyo ametoa neno lake la mwisho kwa Mashabiki na Wanachama wa Klabu hiyo kongwe katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Nabi ameondoka Young Africans akiiongoza Klabu hiyo kutwaa Ubingwa wa Tanzania Bara na Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ mara mbili mfululizo, huku akiifikisha klabu hiyo hatua ya Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika msimu wa 2022/23.
Kocha huyo anayedaiwa kuwa mbioni kutua Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, amewasilisha ujumbe huo kwa Mashabiki na Wanachama wa Young Afrcans kwa njia ya Mtandao ambako anaamini ndiko wengi wanaweza kuupata na kuusoka kwa umakini.
Kocha huyo alijiunga na Young Africans miaka miwili iliyopita akitokea Al Merreikh ya Sudan ameandika: “Ni jambo gumu zaidi ambalo nimelazimika kufanya katika miaka miwili iliyopita, lakini mambo yote mazuri lazima yafike mwisho, Tulipitia nyakati tofauti nyingi tofauti pamoja, kuwa na huzuni hadi furaha na wakati mwingine hasira, lakini kwa neema ya Mungu tuliishi nyakati zisizosahaulika na za kihistoria pamoja.”
“Nilipofika hapa, watu wengi walikuwa na mashaka juu yangu, lakini nilikuja na dhamira moja ya kuwarudishia furaha na shauku kwa klabu yao kubwa na haikuwa rahisi hata kidogo lakini matokeo yamekuwa nje ya matarajio yetu, ndio maana kwanza napenda kuwashukuru wachezaji wangu kwa juhudi zao zote, nimewapenda kama watoto wangu na unapompenda mtu, unamtakia mema na ndivyo ilivyotokea.”
“Pia nataka kuwashukuru wafanyakazi wangu wa kiufundi kwa uvumilivu wao na kazi yao yote pamoja nami, kwa sababu bila nyinyi, hili lisingewezekana, Ningependa pia kuwashukuru wafanyikazi wa Avic Town kwa bidii yao yote, mnafanya kazi bila kuchoka ili kuhakikisha kuwa tuna kila kitu tunachohitaji, na ninyi ni watu wa muhimu sana.”
“Nimshukuru pia Bwana Ghalib kwa usaidizi wake wote katika kipindi cha miaka miwili na nusu iliyopita, asante kwa yote ambayo umenifanyia na asante kwa kunifanya kama mtu wa familia yako, Napenda pia kuwashukuru viongozi na wajumbe wa kamati ya utendaji, mashabiki, hakuna maneno yanayoweza kuelezea kiwango cha upendo nilichonacho kwenu na nguvu zote mlizonipa wakati nipo Yanga SC, Asanteni sana kwa kila kitu.”
“Naumia moyoni kuachana na nyie, lakini ndivyo maisha ya ukocha yalivyo, lia ningependa kuwaambia kuwa sijaondoka sababu ya pesa, bali naamini muumini mzuri anajua kuwa pesa tunayopata katika maisha yetu tayari imepangwa kwa ajili yetu na kwamba kupata pesa hizo leo au kesho haitabadilika.”
“Mwisho, naitakia kila la kheri klabu yangu ya Young Africans SC na ninatumai, kwa rehema za Mwenyezi Mungu, ipo siku nyingine tutavuka tena, Kwaheri familia yangu, ninawakumbuka sana, Nawapenda nyote.”