Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans Nasredden Nabi amesema pamoja na Mashabiki wengi kuamini kikosi chake kilipata matokeo dhidi ya Mtibwa Sugar kwa urahisi, lakini kwake kama Mkuu wa Benchi la Ufundi haamini hivyo.
Mtibwa Sugar ilikubali kupoteza mchezo huo wa Mzunguuko wanne wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kufungwa 3-0 jana Jumanne (Septemba 13), huku ukiwa mchezo wao wa kwanza kupoteza msimu huu.
Kocha Nabi amesema Mtibwa Sugar walionyesha uwezo wa kuikabili timu yake katika dakika 30 za awali na kutoa upinzani mkubwa, hali ambayo ilimlazimu kubadili mbinu ambazo zilimsaidia kupata mabao mawili ya haraka.
Amesema kiufundi mambo hayakuwa rahisi kama inavyodhaniwa, lakini upande wa Mashabiki wana haki wa kuamini hivyo kwa sababu siku zote wamekua wakifurahishwa na matokeo mazuri.
“Ulikua mchezo mgumu sana, japo tumepata ushindi wa mabao 3-0, lakini kiufundi haikuwa rahisi kama inavyochukuliwa na Mashabiki wetu, nafahamu wao wanafurahishwa na matokeo ila kuna kazi kubwa ya kiufundi ilifanywa kupata matokeo haya.”
“Ni wazi inaweza kuonekana tulimaliza mchezo katika kipindi cha kwanza kwa mabao ya Djuma Shaban na Fiston Mayele, lakini dakika 30 za awali zilikua ngumu sana kwa sababu Mtibwa Sugar walikuja na mpango kazi wa kutuzuia ili tusifunge.” amesema Kocha Nabi.
Ushindi huo wa mabao 3-0 unaiwezesha Young Africans kukwea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu, wakifikisha alama 10 wakifuatiwa na Simba SC, Singida Big Stars na Mtibwa Sugar wenye alama 07 kila mmoja.