Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans Nasreddine Nabi, amedhamiria kuzinyakua alama tatu za mchezo watatu wa Ligi Kuu dhidi ya Azam FC, kwa kuhakikisha wachezaj wake wake wanakua FIT kabla ya kushuka Dimbani Septemba 06.
Young Africans itakua nyumbani Uwanja wa Benjamin Mkapa katika mchezo huo, ikiikaribisha Azam FC ambayo itacheza mchezo wake wa kwanza ugenini msimu huu, baada ya kuanzia nyumbani kwa kuifunga Kagera Sugar 2-1 na kulazimishwa sare ya 1-1 dhidi ya Geita gold FC.
Kocha Nabi kwa sasa anawandaa wachezaji wake kwa mazoezi ya viungo (Gym) ili kuwapa utayari wa kupambana katika mchezo huo uliopachikwa jina la ‘Dar es salaam Derby’.
Kikosi cha Young Africans kimeonekana kikifanya mazoezi hayo magumu tangu juzi Jumatatu (Agosti 29) majira ya asubihi katika Gym ya Gymkhana jijini Dar es Salaam na jioni kikiendelea kujijenga kwenye viwanja vya Avic Town ambapo wameweka kambi.
Kocha Nabi, amesema amepanga kuwapeleka nyota wake katika ufukwe wa Coco ili kuendelea kuwanoa kwa sababu anahitaji wawe fiti na tayari kuwakabili Azam FC.
Nabi, amesema anataka kuona wachezaji wake wana pumzi ya kutosha na ndio programu maalumu aliyowaandalia nyota wake katika kipindi hiki cha mapumziko.
“Nahitaji kuwa na kikosi bora na chenye uwezo mkubwa wa kupambana katika dakika zote za mchezo, mazoezi ya viungo ni muhimu kwa sababu yanajenga utimamu wa mwili na kuwaweka imara kuanzia mwanzo hadi mwisho wa mechi,”
“Napambana kujenga kikosi bora kwa sababu nahitaji kuwa na timu imara katika msimu huu ambao tumedhamiria kupambana kupata matokeo mazuri katika michezo yote tutakayocheza,” amesema Nabi.
Kocha huyo ameongeza hataki kuona nyota wake ‘wanakata’ pumzi katikati ya mchezo na endapo hilo litatokea itawaweka kwenye wakati mgumu.
“Ninataka kikosi kiwe na uwezo wa kucheza katika kiwango cha juu, ndio maana tunapambana kuhakikisha wanakuwa imara na vile vile wana pumzi ya kutosha wakati wote, tunahitaji kuwa bora kuliko tulivyokuwa msimu uliopita,” Nabi amesema.
Baada ya mchezo dhidi ya Azam FC, Young Africans itaendelea na maandalizi ya kuwavaa Mabingwa wa Sudan Kusini Zalan FC, katika mchezo wa mkondo wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika utakaochezwa Septemba 10, mwaka huu Uwanja wa Benjamin Mkapa na marudiano yakifanyika katika uwanja huo huo.
Simba inayonolewa na Mserbia Zoran Maki, ndio vinara wa ligi hiyo inayoshirikisha timu 16 wakifuatiwa na mabingwa watetezi Young Africans, kila moja ikijikusanyia alama sita mkononi.