Kocha Mkuu wa Namungo FC, Denis Kitambi amesema anataka kushinda mechi mbili za Ligi Kuu Tanzania Bara zilizobaki ili kumaliza msimu kwenye nafasi ya tano waliyopo hivi sasa.
Kocha huyo alieleza kuwa kwao hayo ni mafanikio makubwa ingawa awali malengo yao yalikuwa ni kubeba ubingwa wa Tanzania Bara.
“Huu ni msimu wa tano kwenye Ligi Kuu ni wazi kwamba tuna uzoefu wa kutosha kupambana na Simba na Yanga katika mbio za ubingwa kwa kuwa imekuwa ngumu basi kumaliza nafasi ya tano itakuwa ni mafanikio kwetu,” amesema Kitambi.
Kocha huyo ambaye aliichukua timu katikati ya msimu baada ya kuondoka kwa Hanour Janza raia wa Zambia, amesema kuwa kilichosababisha washindwe kufikia malengo ni mwenendo mbaya walioanza nao msimu huu.
Amesema pamoja na hayo mikakati yake kwa msimu ujao ni kufanya usajili wa nguvu ili waweze kurudi na nguvu kubwa itakayowawezesha kupigania ubingwa na timu za Simba SC, Young Africans na Azam FC.
Amesema hakuna linaloshindikana kutokana na uwazi uliopo kwenye ligi hivyo amewataka mashabiki wa timu hiyo kuendelea kuiunga mkono timu yao ili msimu ujao waweze kuweka historia kwa kubeba ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Namungo FC kwa sasa inashika nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na alama 39 na imesaliwa na michezo miwili kabla msimu kumalizika ambazo ni dhidi ya Dodoma Jiji FC na Singida Big Stars.