Kaimu Kocha Mkuu wa Namungo FC, Denis Kitambi, ameanza kuipigia mahesabu Simba SC, akisema anawaandaa wachezaji wake kwa mchezo huo mgumu utakaochezwa keshokutwa, Alhamisi (Novemba 09) katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam.
Kitambi amesema hautakuwa mchezo rahisi kwa sababu ya wapinzani wanaokwenda kukutana nao ambao wametoka kujeruhiwa, hivyo ni lazima wawe makini katika safu ya ulinzi kuelekea mchezo huo.
Tayari Kikosi cha Namungo FC kipo mjini kikiendelea kujimarisha kuelekea mchezo dhidi ya Simba SC, ambayo itahitaji kurudisha Imani kwa Mashabiki na Wanachama wake, baada ya kupoteza mbele ya Young Africans kwa mabao 5-1.
Akizungumza jijini Dar es salaam, Kitambi amesema kikubwa anaendelea kufanyia kazi mapungufu ya kikosi chake, kuwahimiza mabeki wake kuwa makini na safu ya ushambuliaji ya Simba SC ambayo tangu kuanza kwa msimu huu haijawahi kutoka uwanjani bila kucheka na nyavu.
Amesema licha ya Simba SC kupoteza mechi ya jumapili (Novemba 05), wataingia kwa tahadhari kubwa kwa sababu ya kutafuta alama tatu muhimu na anaimani wapinzani wao watakuja kivingine kumaliza hasira zao.
“Maandalizi yapo safi, mpaka sasa wachezaji wote wapo vizuri, Kikubwa ni kumheshimu mpinzani wetu na vijana kujituma, hautakuwa mchezo rahisi kwa sababu ya matokeo ya wapinzani wetu kupoteza mechi yao iliyopita.
Simba SC ni timu kubwa ina wachezaji wazuri hata ukiangalia safu ya ushambuliaji iko imara lakini wana mapungufu kwenye ulinzi ninaimani vijana wakipambana tunaweza kupata alama muhimu,” amesema kocha huyo.