Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans Nasreddine Mohamed Nabi, amekiri kushangazwa na taarifa za kutimuliwa kwenye klabu hiyo, ili hali bado anaendelea na majukumu yake.

Jana Jumanne (Oktoba 25) Gazeti la Mwanaspoti liliibuka na taarifa za kutimuliwa kwa kocha huyo kutoka nchini Tunisia, huku likimtaja Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Uganda Vipers SC Roberto Oliveira Gonçalves do Carmo, kuwa mbadala wake.

Nabi amesema aliona taarifa za yeye kuwa kwenye wakati mbaya wa kufukuzwa klabuni hapo, lakini hadi sasa hajapewa taarifa zozote na Uongozi, ambao una jukumu la kuendelea naye ama kusitisha kibarua chake.

Amesema anaendelea na kazi zake za kila siku, na ndio maana hata jana Jumanne (Oktoba 25) alizungumza na Waandishi wa Habari katika Mkutano Maalum wa kuelekea mchezo wa leo Jumatano (Oktoba 26) dhidi ya KMC FC, utakaopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa kuanzia saa moja usiku.

“Kama itatokea nimeondolewa basi ni sawa, kwa kuwa ndio mpira ulivyo, lakini kwa sasa hakuna taarifa rasmi ambayo nimeipokea kutoka kwa viongozi wangu kuhusiana na mimi kuondolewa Young Afrcans.”

“Ninachofahamu bado ni Kocha Mkuu Young Africans na ndio maana utaona kiasi gani nipo katika harakati za kukiandaa kikosi changu kuelekea mchezo wa leo dhidi ya KMC FC.” amesema Nabi

Hadi sasa Nasreddine Mohamed Nabi anashkia rekodi ya Kipekee katika Ligi Kuu Tanzania Bara, kwa kuongoza Young Africans kwenye Michezo 47 bila kufungwa, tangu msimu uliopita 2021/22.

Moses Phiri amtwisha zigo zito Clatous Chama
Habari Kuu kwenye magazeti ya leo Octoba 26, 2022